• Kamanda Mkuu wa IRGC: Fitina mpya dhidi ya Iran ya Kiislamu imesambaratishwa

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, SEPAH (IRGC) amesema fitina mpya iliyoanzishwa dhidi ya Iran imeshindwa na kusisitiza kuwa wananchi waelewa na wenye basira wa Iran wamejitenga na wazusha machafuko, wafanya uharibifu na walamakombo ya maajinabi; na hivyo kupelekea kuhshndwa njama nyengine iliyofanywa dhidi ya Mfumo wa Kiislamu.

Meja Jenerali Mohammad Ali Jaafari amebainisha kuwa kupanga mauaji ni moja ya mipango mikuu iliyoandaliwa na wafanya fitina na mabwana zao katika machafuko ya karibuni nchini Iran, ambapo lengo la kufanya hivyo lilikuwa ni kuibebesha dhima ya mauaji hayo serikali ya Iran; lakini adui amepata pigo jengine tena katika hilo kutokana na utayarifu wa kiusalama uliokuwepo pamoja na basira na kuwa macho wananchi.

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa: akthari ya wahusika wa machafuko waliokuwa kwenye kitovu cha fitina hiyo walikuwa wamepewa mafunzo na wapinga Mapinduzi  na wanafiki; na wote wamejulikana na kutiwa mbaroni.

Meja Jenerali Jaafari ameashiria urafiki wa kizandiki uliodaiwa kuonyeshwa na Marekani, Magharibi na Wazayuni kwa wananchi wa Iran na kuwa kwao bega kwa bega na wahusika wa fitina mpya ya karibuni na kueleza kwamba: laiti kama wazandiki hawa wangekuwa wana uchungu na wanawafikiria wananchi wa Iran, katu wasingewawekea vikwazo wananchi madhulumu wa Iran.

Trump (kushoto) na Netanyahu, miongoni mwa waungaji mkono wakuu wa fitina ya machafuko yaliyotokea nchini Iran

Kamanda Mkuu wa SEPAH amesema, maadui wanaelewa fika kwamba hawawezi kivyovyote vile kuiteteresha kiulinzi Iran na akabainisha kwamba: baada ya vita vya Kujihami Kutakatifu, maadaui wamewekeza na kutumia rasilimali zao zote kwa ajili kuiyumbisha Iran kiutamaduni, kiuchumi na kiusalama, lakini kwa auni na msaada wa Mwenyezi Mungu watashindwa tu katika hilo pia.

Katika siku kadhaa zilizopita baadhi ya watu kwenye miji kadhaa nchini walifanya mikusanyiko na maandamano kulalamikia masuala mbalimbali ikiwemo kutojulikana hatima ya watu waliopata hasara na kupoteza fedha zao katika taasisi za fedha, ughali wa baadhi ya bidhaa na udhaifu wa serikali katika usimamizi. Hata hivyo baadhi ya maandamano hayo yalitumiwa vibaya na watu wenye nia mbaya na wahuni wanaoungwa mkono na baadhi ya nchi za Magharibi, za Kiarabu na utawala wa Kizayuni wa Israel kuzusha fujo na machafuko.../

Jan 03, 2018 15:47 UTC
Maoni