• Tehran mwenyeji wa Mkutano wa 13 wa Mabunge ya Nchi za Kiislamu Wanachama wa OIC

Tehran kuanzia leo Jumamosi ni mwenyeji wa vikao vya utangulizi vya Mkutano wa 13 wa Mabunge ya Nchi za Kiislamu wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Kiislamu (OIC). Vikao vya wataalamu na vya kamati za utekelezaji za Mkutano wa 13 wa Mabunge ya Nchi za Kiislamu Wanachama wa OIC vimeanza kazi leo asubuhi na vitaendelea hadi tarehe 15 mwezi huu.

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) ni taasisi ya pili ya kimataifa  kwa ukubwa baada ya Umoja wa Mataifa na ina nchi 57 wanachama. Jumuiya hiyo kwa hakika ni sauti ya pamoja ya Ulimwengu wa Kiislamu na iwapo itakuwa na msimamo mmoja na kuwa na ushirikiano katika medani za kimataifa inaweza kulinda na kutetea vyema maslahi ya Umma wa Kiislamu na kuwa na nafasi muhimu katika kueneza amai ya kimataifa.

Jina la jumuiya hiyo tangu mwaka 1969 wakati ilipoasisiwa lilikuwa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu sambamba na malengo yake ya wakati huo, na mwaka 2011 jina hilo lilibadilishwa na kuwa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu kwa kutilia malengo makubwa zaidi ya kiuchumi, kijamii, kiutamaduni, kielimu na kadhalika ya nchi wanachama wake. 

Kadhim Jalali ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Utafiti ya Bunge la Iran anasema: Hii leo ulimwengu wa Kiislamu unakabiliana na tatizo la ugaidi, na Jumuiya ya Mabunge ya Kiislamu (PUIC) inaweza kuchukua msimamo imara wa kukabiliana na Daesh na makundi mengine ya kigaidi yanayochafua jina la Uislamu na kuwa na taathira kubwa zaidi katika masuala ya kimataifa. 

Mkutano wa Mabunge ya Kiislamu mjini Tehran

Mkutano wa sasa wa Mabunge ya Kiislamu mjini Tehran unawakutanisha pamoja wawakilishi wa mabunge 41 ya nchi Asia na Afrika. Mkutano huu ni sehemu ya jitihada za kidiplomasia za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran za kutaka kuimarisha amani, kupanua ushirikiano na kujenga umoja na mshikamano katika Umma wa Kiislamu kupitia wawakilishi wa mataifa ya Waislamu. Iran daima imekuwa ikifanya jitihada kubwa za kutumia njia za kidiplomasia na mashauriano hususan kupitia mabunge kwa ajili ya kuimarisha amani, ushirikiano na kubuni njia mpya za ustawi na maendeleo. Jitihada hizo zinafanyika kupitia mchango na nafasi ya Tehran katika taasisi na jumuiya mbalimbali kama Jumuiya ya Mabunge ya Kiislamu (PUIC) na Jumuiya ya Mabunge la Asia (APA). 

Maudhui ya Palestina na Quds tukufu na kadhia kama ugaidi na haki za binadamu ni masuala yenye umuhimu mkubwa kwa nchi za Kiislamu na yanazua wasiwasi katika upeo wa Ulimwengu wa Kiislamu na hata katika medani ya kimataifa. Mbali na masuala hayo, katika kipindi hiki nyeti na muhimu, Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) na Jumuiya ya Mabunge ya Kiislamu zinalipa umuhimu mkubwa suala la kutekelezwa kikamilifu makubaliano na mikataba ya kuharibiwa kabisa silaha za nyuklia. Katika kipindi cha sasa ambapo Marekani inaweka vizuizi katika utekelezaji wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, ni muhimu sana kwa jamii ya kimataifa hususan nchi za Kiislamu kutilia maanani tishio halisi la nyuklia zikiwemo silaha za nyuklia za utawala haramu wa Israel na vilevile umuhimu wa kutekelezwa makubaliano ya kuharibiwa silaha hizo hatari kote duniani.

Alaa kulli hal, juhudi za pamoja za mabunge ya nchi za Kiislamu katika nyanja hizo zote zinaweza kuimarisha msimamo wa Umma wa kutatua migogoro na matatizo ya kutwishwa kutoka nje ya nchi za Kiislamu.

Kwa msingi huo inatarajiwa kwamba, washiriki katika Mkutano wa 13 wa Mabunge ya Nchi za Kiislamu watatilia maanani changamoto, migogoro na masuala muhimu ya Umma wa Kiislamu.    

Jan 13, 2018 12:05 UTC
Maoni