Jan 13, 2018 14:15 UTC
  • Kazem Jalali: Palestina inapaswa kubakia kuwa kadhia muhimu zaidi katika jumuiya ya mabunge ya OIC

Mkuu wa mkutano wa 39 wa Kamati ya Utendaji Jumuiya ya Mabunge ya Nchi za Kiislamu wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) amesisitiza kuwa, kadhia ya Palestina inapaswa kuwa suala linalopewa kipaumbele zaidi katika utendaji wa Jumuiya ya Mabunge ya Nchi za Kiislamu.

Kazem Jalali amesema hayo leo hapa mjini Tehran na kulaani vikali uamuzi wa hivi karibuni wa Rais Donald Trump wa Marekani wa kuitangaza Beitu-Muqaddas kuwa mji mkuu wa utawala dhalimu wa Israel.

Mkuu wa mkutano wa 39 wa Kamati ya Utendaji  Jumuiya ya Mabunge ya Nchi za Kiislamu amesema kuwa, kwa njama yake hiyo Trump anafuatilia suala la kutoa pigo kwa heshima na umoja wa Waislamu.

Bendera ya Palestina

Kazem Jalali amesema pia kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitaacha kufanya juhudi za kila namna ili kuzuia uingiliaji na upenyaji wa madola ajinabi katika masuala ya nchi za Kiislamu. 

Wakati huo huo, Tehran kuanzia leo Jumamosi ni mwenyeji wa vikao vya utangulizi vya Mkutano wa 13 wa Mabunge ya Nchi za Kiislamu wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Kiislamu (OIC).

Vikao vya wataalamu na vya Kamati za Utekelezaji za Mkutano wa 13 wa Mabunge ya Nchi za Kiislamu Wanachama wa OIC vimeanza kazi leo asubuhi na vitaendelea hadi tarehe 15 mwezi huu.

Tags

Maoni