Feb 05, 2018 16:31 UTC
  • Qassemi: Iran haitakubali sharti lolote lile kuhusiana na safari ya Rais wa Ufaransa mjini Tehran

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran haitakubali sharti lolote lile kwa ajili ya safari ijayo ya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa hapa nchini.

Bahram Qassemi amesema hayo leo katika mkutano wake na waandishi wa habari wa ndani na wa nje ambapo akizungumzia tetesi za kuwekewa masharti Iran kwa ajili ya safari ijayo ya Rais wa Ufaransa hapa Tehran amesema kuwa, katika kipindi cha miongo minne iliyopita, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeonyesha inafuata njia gani katika mahusiano na tawala nyingine.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha kwamba, licha ya kuweko uhusiano unaokuwa baina ya Iran na Ufaransa, lakini Paris haiko katika nafasi ya kuiwekea masharti Tehran.

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa 

Bahram Qassemi amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran si taifa la kukubali masharti na inachukua maamuzi yake yenyewe kuhusiana na sera za ndani na za kigeni.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema bayana kwamba, suala linalozungumziwa la masharti ya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa kwa ajili ya kufanya safari hapa nchini si sahihi na si la mahala pake na katu halina nafasi katika siasa za Jamhuri ya Kiislamu.

Bahram Qassemi amezungumzia  suala la kuendelea kuweko kijeshi Uturuki katika ardhi ya Syria  na kusema kwamba, operesheni hiyo ya kijeshi inapaswa kusimamishwa haraka na kuheshimiwa mamlaka ya kujitawala Syria.

Tags

Maoni