Feb 08, 2018 03:57 UTC
  • Russia yatoa indhari kuhusu matokeo yasiyotabirika endapo makubaliano ya nyuklia na Iran yatavunjika

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergei Lavrov ameonya kuwa kuvunjika makubaliano ya nyuklia na Iran kunaweza kuwa na matokeo yasiyoweza kutabirika.

Shirika la habari la Interfax limemnukuu Lavrov akitoa indhari kwa mara nyengine tena kwamba hatua zinazochukuliwa kwa madhumuni ya kuyavunja makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) zitakuwa na matokeo mabaya.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ameongeza kuwa Umoja wa Ulaya nao pia hauridhishwi na misimamo ya Marekani kuhusiana na makubaliano ya nyuklia na Iran; kwa hivyo Washington inapaswa iwe makini juu ya suala hilo.

Wakati huohuo Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergei Ryabkov, naye pia ametahadharisha kuwa hatua za Marekani za kutaka hati ya JCPOA ifanyiwe mabadiliko mwishowe zitapelekea kusambaratika makubaliano hayo; na Moscow haitotaka kwa namna yoyote ile ihusike katika mchakato huo haribifu.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa makubaliano ya JCPOA ni mkataba wa kimataifa uliopasishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kwamba hati ya makubaliano hayo haitapunguzwa wala kuongezewa chochote.../

 

Tags

Maoni