Feb 08, 2018 07:18 UTC
  • Iran: Syria itakombolewa karibuni hivi

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (SEPAH) amesema kuwa, baada ya kusafishwa kabisa magaidi wa kundi la Daesh (ISIS) nchini Iraq, karibuni hivi dunia itashuhudia Syria nayo ikikombolewa kikamilifu.

Meja Jenerali Mohammad Ali Jafari amesema hayo usiku wa kuamkia leo katika mkoa wa Kerman wa kusini mwa Iran na kuongeza kuwa, baada ya Iran kufanikiwa kuwathibitishia walimwengu nguvu zake na kusimama kwake imara mbele ya njama za maadui, sasa wananchi wa Lebanon, Iraq, Palestina, Yemen na Syria nao wamepata nguvu za kusimama kidete kupambana na maadui zao.

Wanajeshi wa Syria na picha kubwa ya Rais Bashar al Assad

 

Amesema, baada ya mataifa mengine kuona mafanikio ya Iran ya kusimama imara kukabiliana na maadui, yamekuwa na imani sana kwa kambi ya muqawama na yamepata yakini kuwa yanaweza kusimama kidete mbele ya mabeberu na watawala madikteta na kufanikiwa kukomboa haki zao.

Meja Jeneral Jafari pia amegusia mafanikio mengi muhimu ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na kuongeza kuwa, kueneza utamaduni wa muqawama katika eneo hili na duniani kwa ujumla, kupanua harakati ya mwamko wa Kiislamu katika ukanda huu, kuvunja udhibiti wa maadui na kambi za Mashariki na Magharibi duniani ni miongoni mwa mafanikio makubwa ya Mapinduzi ya Kiislamu katika upeo wa kiroho na kimaanawi; mafanikio ambayo yanawachukiza mno maadui.

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran SEPAH aidha amesisitiza kuwa, kusimama imara kupambana na dhulma, uistikbari na ukandamizaji ni miongoni mwa mafunzo muhimu ya Imam Khomeini MA, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, mafunzo ambayo yameendelea kutekelezwa na kulindwa vizuri na Mapinduzi ya Kiislamu hadi leo hii.

Tags

Maoni