Feb 09, 2018 14:25 UTC
  • Araqchi:Utawala wa Kizayuni, Saudia, na Marekani ni chanzo cha migogoro Mashariki ya Kati

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amelaani vikali sera za Utawala wa Kizyauni wa Israel, Saudi Arabia na Marekani na kusema ndio chanzo cha migogoro na vita Mashariki ya Kati.

Sayyed Abbas Araqchi ameyasema hayo pembizoni mwa Kongamano la Euromoney mjini Paris Ufaransa huku akisisitiza kuwa, Iran imekuwa katika mstari wa mbele wa kupambana na ugaidi na kurejesha uthabiti na amani katika eneo.

Araqchi aidha amesema hakuna uhusiano wowote baina ya nafasi ya Iran na mapatano ya nyuklia ya mwaka 2015 kati yake na madola sita makubwa duniani ya kundi la 5+1.

Araqchi amesema kuwa Iran inajitahidi kurejesha utulivu katika eneo na hilo halina uhusiano wowote na mapatano ya nyuklia ambayo rasmi yanajulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji, JCPOA.

Mapatano hayo yalifikiwa baina ya Iran na wanachama watano wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na Ujerumani. Kwa mujibu wa mapatano hayo, Iran ilipaswa kuondolewa vikwazo vyote vinavyohusiana na kadhia ya nyuklia mkabala wa kupunguza shughuli zake za nishati ya nyuklia.

Mfalme Salman wa Saudia akimpa mkono mke wa Rais Trump wa Marekani mjini Riyadh

Pamoja na hayo, Rais Donald Trump wa Marekani amekuwa akijaribu kuvuruga mapatano hayo kwa kudai kuwa ni mapatano mabaya zaidi ambayo Marekani imewahi kushiriki.

Lakini kinyume na madai hayo ya Trump, wakuu wa  Umoja wa Ulaya na Umoja wa Mataifa wameyataja mapatano hayo kuwa ushindi wa kidiplomasia kwa maslahi ya usalama wa kieneo na kimataifa. Aidha wameionya Marekani kuwa haiwezi kuchukua hatua ya upande mmoja ya kujiondoa katika mapatano hayo. Marekani imekuwa ikitaka kufanyike mazungumzo mapya kuhusu mapatano hayo ili kadhia ya makombora ya kujihami ya Iran ijumlishwe humo. Hata hivyo Iran imesisitiza kuwa haiwezi kufanya mazungumzo mapya kuhusu mapatano hayo wala kadhia ya makombora yake ya kujihami.

Tags

Maoni