• Iran yasema ipo tayari kusaidia operesheni za kulinda amani duniani

Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa ameueleza umoja huo juu ya utayarifu wa Tehran wa kuchangia na kusaidia operesheni za kulinda amani duniani.

Gholamali Khoshroo aliyasema hayo jana Jumanne na kuongeza kuwa, serikali ya Tehran ipo tayari kuongeza mchango wake wa kilojistiki na wanajeshi kwenye operesheni za kudumisha amani katika nchi mbali mbali duniani.

Akihutubia Kamati Maalumu ya UN ya Operesheni za Kulinda Amani, Khoshroo amebainisha kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inawapongeza wanajeshi waliotumwa katika nchi mbalimbali kudumisha amani na kuhatarisha maisha yao.

Mwanadiplomasia huyo wa Iran amesema Tehran ipo tayari kutoa mchango wa kutuma waangalizi wa kijeshi, askari, polisi na hata wataalamu wake katika operesheni za kulinda amani za UN.

Askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa

Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa hata hivyo ameonya kuwa, umoja huo unapaswa kujiepusha na uingiliaji wa kijeshi wa nchi ajinabi katika nchi nyingine kwa kisingizio cha kuwalinda raia. 

Kadhalika amewataka wanajeshi na maafisa wengine wa UN wanaotumwa katika sehemu mbalimbali duniani kudumisha viwango vya juu vya maadili, na hususan kujiepusha na jinai za kingono zilizovipaka matope vikosi hivyo vya askari wa kofia buluu.  

Tags

Feb 14, 2018 08:09 UTC
Maoni