• Baada ya kufanikiwa ushirikiano wao katika vita dhidi ya ugaidi, sasa Iran na Iraq zatiliana saini mapatano maalumu ya kijeshi

Naibu Waziri wa Ulinzi wa Iran na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi ya Iraq wamekutana na kutiliana saini mapatano maalumu ya kijeshi.

Hujjatullah Qureshi, Naibu Waziri wa Ulinzi wa Iran na ujumbe anaoandamana nao, jana (Jumapili) alionana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi ya Iraq mjini Baghdad na pande mbili zikabadilishana mawazo kuhusu masuala ya kijeshi na kiulinzi ya nchi zao.

Katika mazungumzo hayo, pande mbili zimetiliana saini mapatano maalumu ya kijeshi huku Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikisisitiza kuwa iko tayari kuisaidia Iraq kwa silaha na vifaa vya kijeshi.

Mpaka wa Iran na Iraq

 

Pande hizo mbili zimekubaliana pia kuunda kamati mbalimbali za kufuatilia na kufanikisha utekelezaji wa kivitendo wa mapatano hayo.

Itakumbukwa kuwa mwezi Julai 2017, Wizara za Ulinzi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Iraq zilitiliana saini hati wa mapatano kwa ajili ya kushirikiana kiulinzi na kijeshi katika uga mpana zaidi.

Miongoni mwa maeneo ambayo nchi mbili za Iran na Iraq zinashirikiana ni pamoja na vita dhidi ya ugaidi na misimamo mikali, usalama mipakani na masuala ya mafunzo ya kijeshi, misaada ya kilojistiki na kiufundi na masuala mengine yanayohusiana na ulinzi na jeshi.

Tags

Feb 19, 2018 03:04 UTC
Maoni