• Zarif: Magaidi wanakaribia mipaka ya Iran na Russsia

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitizia ulazima wa kutoingilia madola ya kigeni mambo ya ndani ya nchi za Mashariki ya Kati na kuheshimu haki na mamlaka ya kujitawala nchi za eneo hilo.

Mohammad Javad Zarif ameyasema hayo mjini Moscow Russia katika Kongamano la Valdai la Kujadili Matukio ya Mashariki ya Kati na kusema: "Pamoja na kuwa magaidi wa Daesh (ISIS) wameangamizwa nchini Syria na Iraq, lakini changamoto itokanayo na ugaidi inaendelea kwani leo magaidi hao wamefika karibu na ardhi za Russia na Iran katika eneo la kaskazini mwa Afghanistan."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitizia wajibu wa kuwepo ushirikiano wa nchi mbali mbali katika kukabiliana na ugaidi na misimamo mikali Mashariki ya Kati. Ameongeza kuwa Iran inashirikiana na serikali za Iraq na Syria pamoja na washirika wengine katika eneo hili hasa Russia na mkondo huu umeweza kusaidia sana katika kukabiliana na magaidi.

Zarif amesema, mgogoro wa Syria unahitajia suluhisho la kisiasa na kuongeza kuwa, hatua ya Marekani kutumia askari wa niaba nchini Syria ni jambo ambalo ni hatari kwa Marekani yenywe na pia kwa eneo hili.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif (kushoto) na mwenzake wa Russia Sergei Lavrov mjini Moscow, 19/02/2018

Aidha Zarif amesisitiza kuhusu nafasi ya Iran na Russia katika kutatua migogoro na mapigano Mashariki ya Kati na kuipongeza Russia kwa muelekeo wake wa kiistratijia katika eneo la magharibi mwa Asia.

Amesema uwepo wa Russia katika eneo hili ni jambo linaloweza kutumiwa kuleta kigezo kipya katika eneo la Ghuba ya Uajemi. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia ameashiria mgogoro wa Yemen na kusema kuwa nao unahitaji suluhisho la kisiasa. Ameongeza kuwa, Iran daima imekuwa ikijitahidi sana kutafuta suluhisho la kisiasa katika migogoro yote ya eneo hili.

Feb 19, 2018 15:48 UTC
Maoni