• Duru mpya ya harakati za kisiasa kati ya Iran na Ulaya

Tehran leo Jumatano ni mwenyeji wa viongozi wawili wa Ulaya. Sigrid Kaag Waziri wa Mambo ya Nje wa Uholanzi jana usiku aliwasili hapa Tehran kwa ajili ya mazungumzo na viongozi wa Iran.

Sambamba na ziara hiyo, Alfonso Dastis Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania pia atakuwa na mazungumzo hapa Tehran na viongozi wa Iran kuhusu mahusiano ya pande mbili na yale ya kieneo na kimataifa. Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania amesema mara baada ya kuwasili hapa Tehran kuwa: Madrid mbali na kuimarisha uhusiano wake wa kiuchumi itaboresha pia muundo wa mashauriano ya kisiasa kati yake na Iran. 

Alfonso Dastis, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania  

Jean -Yves Le Drian  Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa pia jana alitangaza kuwa atafanya ziara hapa nchini siku chache zijazo. 

Wakati huo huo Abbas Araqchi Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamuu ya Iran Anayehusika na Masuala ya Kisiasa ameelekea ziarani  mjini London akiongoza ujumbe wa kisiasa wa nchi hii kwa lengo la kushiriki kwenye mazungumzo ya kisiasa kati ya Iran na Uingereza. Araqchi kesho Alhamisi anatazamiwa kuhutubia Taasisi ya Chatham House mjini London. 

 Abbas Araqchi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Anayehusika na Masuala ya Kisiasa 
 

Miamala hiyo ina umuhimu katika pande mbili za kieneo na kimataifa kwa sababu inaweza kuwa mwanzo wa matukio muhimu katika uhusiano kati ya Iran na nchi za Ulaya. Ni zaidi ya mwaka mmoja sasa ambapo Trump amekuwa akitekeleza hatua mbalimbali za ukwamishaji ili kuvuruga makubaliano ya nyuklia ya JCPOA huku tukishuhudia pia Marekani ikiendeleza mashinikizo ili kuzusha ufa kati ya Iran na nchi za Ulaya. Hata kama Umoja wa Ulaya hadi sasa umeonyesha kutotaka kupoteza matunda yaliyopatikana katika makubaliano hayo kwa kuathiriwa na matakwa ya Trump, lakini Umoja huo haujakuwa wazi kwa kiasi kikubwa kimsimamo kuhusiana na masuala mengineyo yanayohusu makubaliano ya JCPOA.   

Taasisi ya Carnegie imeandika katika uchambuzi wake kuwa: Iran ni fursa nzuri kwa Ulaya na Ulaya haitaki kuipoteza fursa hiyo. 

Pamoja na hayo badhi ya nchi za Ulaya zimekuwa zikiiunga mkono Marekani katika madai yake dhidi ya Iran licha ya kusisitiza juu ya nafasi muhimu ya Iran katika kulinda uthabiti na amani katika eneo. Aidha nchi hizo zimekuwa zikitoa tafsiri zinazoshabihiana katika kudhihirisha kuwa uwezo wa makombora wa Iran ni tishio; jambo ambalo halina uhusiano wowote na nchi nyingine. 

Bahram Qassemi Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran jana alijibu matamshi ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa na Uingereza waliosema kwamba wana wasiwasi na mradi wa ulinzi wa makombora ya Iran na kuyataja matamshi hayo kuwa yasiyo na halalilisho lolote la kimantiki. Qassemi aliongeza kuwa: Iran inaichukulia misimamo kama hiyo kuwa kinyume na maadili na ni kitendo ambacho si cha uwajibikaji. 

Sayyid Abbas Araqchi Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Anayehusika na Masuala ya Kisiasa pia huko nyuma aliwahi kusema kuwa mitazamo ya baadhi ya nchi za Ulaya ya kutoa upendeleo kwa Rais Donald Trump wa Marekani ili  nchi hiyo isalie katika makubaliano ya nyuklia ya (JCPOA) ni mitazamo potofu kikamilifu na ni wazi kuwa hatua hizo zitakuwa na matokeo hasi.

Feb 21, 2018 08:06 UTC
Maoni