• Rais Rouhani aitaka Saudia ihitimishe mauaji yake dhidi ya raia wa Yemen

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameitaka Saudi Arabia na washirika wake waache mchezo wao wa kuilaumu na kuituhumu Iran kuhusiana na mgogoro wa Yemen na badala yake wahitimishe mauaji wanayoyafanya dhidi ya raia wa nchi hiyo.

Rais Rouhani amesema hayo leo katika mazungumzo yake hapa mjini Tehran na Bi Sigrid Kaag, Kaimu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Uholanzi aliyeko hapa nchini kwa safari rasmi ya kikazi na kubainisha kwamba, Saudia na washirika wake wanapaswa kukomesha mauaji huko Yemen ili kutoa fursa ya kusonga mbele juhudi za kuupatia ufumbuzi mgogoro huo kwa njia za amani.

Rais Rouhani amekanusha vikali madai kwamba, Tehran imekuwa ikipeleka makombora nchini Yemen na kusema kwamba, madai hayo ni ya urongo na hayana maana.

Yemen inavyohariobiwa na mashambulio ya anga ya Saudia

Amesema kuwa, kuituhumu Iran katu hakuwezi kusaidia kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Yemen bali kuna haja ya nguvu kuelekezwa katika juhudi za mazungumzo ya kuhitimisha vita na kupelekwa misaada ya kibinadamu kwa raia wa Yemen walioko katika hali mbaya.

Kwa upande wake Bi Sigrid Kaag, Kaimu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Uholanzi ameashiria msimamo wa Umoja wa Ulaya wa kuendelea kufungamana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na nafasi kubwa ya makubaliano hayo katika kustawisha uhusiano kati ya pande mbili.

Aidha amesema nchi yake inatambua haki ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kuimarisha uwezo wake wa kiulinzi na kwamba, mpango kama huo ni halali.

Tags

Feb 21, 2018 15:22 UTC
Maoni