• Indhari ya kuvunjika makubaliano ya JCPOA, kutoka Vienna hadi Tehran

Njama za Rais Donald Trump wa Marekani za kutaka kuyafanya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yasiwe na itibari na hata nchi yake kujitoa katika makubaliano hayo, kwa mara nyingine tena yamekuwa mambo makuu katika masuala yanayohusiana na JCPOA.

Yukiya Amano, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) Jumatatu ya jana alitoa taarifa ambayo pamoja na mambo mengine ilitahadharisha juu ya matokeo mabaya ya mashinikizo ya Marekani ya kutaka kuyakwamisha makubaliano hayo. Akizungumza katika kikao cha Bodi ya Magavana ya wakala wa IAEA mjini Vienna Austria Amano alisema bayana kwamba: 

Makubaliano ya nyuklia ya Iran ni ishara ya mafanikio makubwa katika uga wa harakati za nyuklia na kwamba, kama  makubaliano hayo yatavunjika litakuwa "pigo kubwa" kwa hatua za ukaguzi na udhibiti wa miradi ya nyuklia na utekelezaji wa maamuzi ya pamoja ya pande kadhaa. 

Makao makuu ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomikia IAEA Vienna Austria

Sambamba na tamko hilo la Amano huko Vienna, mjini Tehran nako suala la matokeo mabaya ya Marekani kutotekeleza majukumu yake na kutofungamana na makubaliano ya nyukllia ya JCPOA lilikuwa moja ya maudhui muhimu katika mazungumzo ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ufaransa na viongozi mbalimbali hapa nchini.

Katika mazungumzo yake ya jana hapa mjini Tehran na Jean-Yves Le Drian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ufaransa, Rais Hassan Rouhani wa Iran sambamba na kusisitiza udharura wa kulindwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kwa ajili ya ustawi wa kiusalama, utulivu na ushirikiano wa kieneo alitahadharisha kwamba: Kuvunjika makubaliano hayo kutakuwa na majuto kwa wote.

Kwa upande wake Jean-Yves Le Drian , Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ufaransa amesisitiza katika mazungumzo yake hapa mjini Tehran kwamba, Ulaya na hasa Ufaransa inaheshimu na kufungamana na makubaliabno hayo na inapenda kuona yakitekelezwa licha ya kuweko mashinikizo ya Marekani.

Mazungumzo ya Rais Rouhani na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian-Tehran 5/03/2018.

Pamoja na hayo baadhi ya mienendo na matamshi ya viongozi wa Ulaya katika kutekelezwa makubaliano ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji JCPOA  pamoja na kuathiriwa kwao na mashinikizo ya Marekani ni mambo ambayo yamekuwa yakikosolewa na Iran.

Sabah Zanganeh, mtaalamu wa mahusiano ya kimataifa anaamini kwamba, Marekani inafanya njama za kusambaratisha muhtawa wa makubaliano ya JCPOA na kwa kutumia mbinu nyingine kama kuongeza vikwazo dhidi ya Iran ipanue zaidi wigo wa mashinikizo.

Kuna nukta kadhaa muhimu katika uwanja huo ambapo baadhi yake ni za kukariri lakini bado kuna haja ya kuzitilia mkazo. Mosi, chombo kinachopaswa kuwa marejeo ya kufuatilia na kueleza mtazamo kuhusiana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA si Marekani wala ikulu ya rais wa nchi hiyo, White House, bali ni Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) ambao kupitia Mkurugenzi Mkuu wake Yukiya Amano, umekuwa ukitangaza mara kwa mara kwamba, Iran imeheshimu na kutekeleza kikamilifu makubaliano hayo.

Kamati ya pamoja ya JCPOA

Pili, makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ni kwa maslahi ya Iran na kama yatatiwa dosari kupitia misimamo isiyo na busara na ya upande mmoja ya Marekani, bila shaka Iran nayo itachukua maamuzi yatakayoendana na mienendo isiyo na mantiki ya Washington. Nukta ya tatu ni kwamba, aina ya majibu na uchukuaji maamuzi katika uwanja huu unapaswa kutoka kwa nchi za Umoja wa Ulaya.

Ukweli ni kwamba, siasa za uharibifu za Rais Donald Trump wa Marekani na Umoja wa Ulaya zinatia wasiwasi. Hivyo basi, kama hakutachukuliwa hatua katika uwanja huu na Umoja wa Ulaya kutochagua njia yake ambayo iko tofauti na vitendo visivyo vya kimantiki vya Marekani, bila shaka wenyewe ndio utakaoshindwa katika mchezo huu mchafu wa kisiasa.

Mar 06, 2018 12:04 UTC
Maoni