• Kiongozi: Kujishughulisha Iran na masuala ya eneo hakuna uhusiano wowote na Marekani na Ulaya

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyed Ali Khamenei amesema: wakati Marekani inajiingiza kila mahali kwa kuzusha fitina na kufanya uharibifu, kila mara inatilia shaka kuwepo na kujishughulisha Iran na masuala ya eneo la Mashariki ya Kati.

Ayatullah Khamenei ameyasema hayo leo asubuhi katika hotuba aliyotoa mbele ya hadhara ya maelfu ya malenga na wasomaji mashairi ya kuwasifu Ahlul-Bayt (AS) kwa mnasaba wa maadhimisho ya kuzaliwa Siddiqatul-Kubra, Bibi Fatimatu-Zahra (SA), binti mpenzi wa Bwana Mtume Muhammad SAW. 

Akitoa jibu kwa kauli za viongozi wa Marekani na Ulaya za kupinga kuwepo na kushughulikia Iran masuala ya eneo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amehoji kwa kusema: "Kwani sisi tunapaswa kuomba idhini kwa Marekani kwa ajili ya kuwepo katika eneo? Akafafanua zaidi kwa kusema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inapaswa kufanya mazungumzo na serikali za nchi za eneo kwa ajili ya kuwepo kwake katika eneo, si na Wamarekani. Pale tutakapotaka kuwepo ndani ya Marekani tutafanya mazungumzo na nyinyi."

Akiwajibu pia viongozi wa UIaya walioeleza kwamba wangependa kufanya mazungumzo na Iran kuhusu kujishughulisha kwake na masuala ya eneo, Ayatullah Khamenei alitilia mkazo tena nukta hiyohiyo kwa kuhoji: Suala hili lina uhusiano gani na nyinyi?

Sehemu moja ya hadhirina

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, miaka 40 ya njama mtawalia na zisizo na mfano za maadui dhidi ya taifa la Iran na wakati huohuo kustawi na kuzidi kunawiri siku baada ya siku mti mzuri wa Mapinduzi ni jambo la fahari na la kujivunia na ni ishara ya fadhila na rehma za Mwenyezi Mungu; na akafafanua kuwa: tangu miezi kadhaa nyuma maadui wa Iran walikuwa wamekaa kwenye vituo vyao vya kubuni fikra na kupanga kwa ajili ya miezi mitatu ya mwisho ya mwaka mpango ambao kwa dhana yao utaisambaratisha moja kwa moja Jamhuri ya Kiislamu.

Ayatullah Khamenei amesema, kuzungumzia masuala kama "uadilifu wa kijinsia" kunakoshuhudiwa katika matamshi ya Wamagharibi ni kitu cha udhahiri tu na kisicho na ukweli wowote. Akiashiria matamshi yaliyotolewa miezi ya karibuni na wanawake wengi wenye hadhi huko Magharibi, waliokiri kwamba wamefanyiwa vitendo vya udhalilishaji na kutumiwa vibaya kijinsia maofisini, Ayatullah Khamenei amesema: kwa kutumia Hijabu, Uislamu umeuziba mwanya huo wa upotofu; kwa hivyo Hijabu ni ngao na kinga ya mwanamke.

Wanawake wa Kiirani ambao ni wabunge katika bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha pia kwamba bendera ya uhuru wa utambulisho na utamaduni wa wanawake inapeperushwa na wanawake wa Kiirani; na akafafanua kwa kusema: sambamba na kuchunga Hijabu, wanawake wa Kiirani wameuonyesha ulimwengu kuwa ni watu wenye uhuru wa utambulisho na utamaduni na kuutangazia kitu kipya, nacho ni kwamba mwanamke anaweza kushiriki kikamilifu na kutoa mchango athirifu katika medani za kijamii huku akiwa amechunga Hijabu na staha yake na kujiepusha na kutumiwa vibaya na wanaume maajinabi na wenye uchu.

Aidha ameongeza kuwa: umahiri ulioonyeshwa na Mapinduzi ya Kiislamu ni kwamba leo hii wanawake wa Kiirani ni miongoni mwa wataalamu na shakhsia bora kabisa wa kiutamaduni. Kwa sababu kabla ya Mapinduzi hali haikuwa hivyo, kwani idadi ya wanawake wenye hadhi za juu kielimu na kiutamaduni ilikuwa haba mno.../ 

Tags

Mar 08, 2018 16:36 UTC
Maoni