• Kiongozi Muadhamu: Tuko katikati ya medani kubwa ya vita

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria jinsi kambi inayoipinga Jamhuri ya Kiislamu ilivyoanzisha vita vikubwa na tata sana dhidi ya taifa la Iran na kusisitiza kuwa, hivi sasa tupo katikati ya medani ya vita vikubwa ambavyo upande wake mmoja kuna mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na upande wa pili kuna kambi kubwa yenye nguvu ya maadui.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo leo asubuhi (Jumatano) wakati alipoonana na waziri, maafisa na wafanyakazi wa Wizara ya Usalama wa Taifa ya Iran na kuongeza kuwa, licha ya mashirika ya kijasusi ya kambi ya maadui kuwa na suhula nyingi sana, lakini hadi hivi sasa yameshindwa kulifanya chochote taifa la Iran. Amesema: "Tab'an kama tutakumbwa na mghafala katika vita hivyo, tutashindwa; na kama tutapuuza mambo na kuyadharau, tutapata hasara."

Mkutano wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na maafisa usalama

 

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa ufafanuzi zaidi kuhusu vita tata vya kijasusi vilivyopo dhidi ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kwa kusema: "Katika vita hivi kunatumika mbinu na mizungu mingi kama vile 'kupenya na kuiba taarifa za kijasusi' na 'kubadilisha mahesabu ya wachukuaji maamuzi' na 'kubadilisha imani za watu' hadi 'kuzusha migogoro ya kifedha na kiuchumi'  na 'kuzusha hatari za kiusalama'."

Amezungumzia pia suala la hivi karibuni la kupanda kiholela thamani ya fedha za kigeni humu nchini na kusema: Wakati tunapoyaangalia kwa umakini na kwa kina zaidi masuala hayo tutaona wazi namna taasisi na mashirika ya kijasusi ya maadui yalivyohusika.

Ayatullah Khamenei aidha amesema: Kuna wajibu wa kusimama imara kukabiliana na njama za kambi hiyo ya maadui ambapo mbali na kuwa na ratiba za kujilinda, tuwe pia na ratiba za kushambulia kwa namna ambayo chombo chetu cha usalama kiwe ndicho chenye nguvu za juu katika vita hivyo.

Apr 18, 2018 16:35 UTC
Maoni