Apr 19, 2018 08:20 UTC
  • Vita vikubwa na tata vya harakati iliyo dhidi ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kwa mtazamo wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu

Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu mapema jana alikutana na kufanya mazungumzo na waziri, maafisa na wafanyakazi wa Wizara ya Usalama wa Taifa ya Iran.

Akihutubia jana asubuhi mbele ya hadhara ya waziri, maafisa na wafanyakazi wa Wizara ya Usalama wa Taifa ya Iran, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliashiria vita vikubwa na tata vya kambi inayokabiliana na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na akayataja mashirika ya ujasusi ya upande wa pili kuwa chanzo kikuu cha makabiliano hayo. 

Kiongozi Muadhamu akiwasili kutoa hotuba 

Akibainisha malengo ya vita hivyo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliashiria taathira za vita hivyo tata na kuongeza kuwa: Sisi tupo katikati ya medani kubwa ya vita  ambavyo kwa upande mmoja ipo Jamhuri ya Kiislamu; na kwa upande wa pili kuna harakati kubwa na yenye nguvu ya maadui.  Moja ya malengo makuu ya maadui katika eneo hili ni kuibua migogoro na kuyagombanisha mataifa ya eneo hili katika migogoro mikubwa kupitia ushawishi wao na kujipenyeza katika ngazi za kiusalama, kiintelijensia, kiuchumi na kiutamaduni. 

 Tukitupia jicho miamala, maamuzi na hatua ambazo zimekuwa zikichukuliwa na Marekani katika siasa zake za nje katika kipindi cha miaka kadhaa na khususan katika miongo ya karibuni tunashuhudia kwamba lengo kuu la wanasiasa wa nchi hiyo limekuwa ni kupata njia ya kuweza kujipenyeza katika Mfumo wa Kiislamu na kuingilia usalama wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.  Kujipenyeza na kuingilia kati ni maneno mawili muhimu ambayo Kiongozi Muadhamu amekuwa akiyasisitizia mara kwa mara  kuhusiana na jambo hilo na katika kuibainisha siasa za Marekani kuhusiana na Iran na eneo hili kwa ujumla. 

Njama mbalimbali zimekuwa zikitekelezwa na mashirika ya ujasusi ya Magharibi dhidi ya Iran

Kuhusiana na suala hilo, hotuba ya jana ya Kiongozi Muadhamu ilikuwa na  nukta kuu kadhaa ambazo zinakumbushia udharura wa kuendelea kuwa macho mbele ya mipango na njama za muda mrefu za Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati. Kiongozi Muadhamu aidha alibainisha taathira na ukubwa wa vita hivyo na kuashiria mbinu mbalimbali zinazotumiwa ikiwemo kujipenyeza na kuiba taarifa, kubadili mahesabu ya wachukuaji maamuzi na kubadili pia imani za wananchi na hivyo kusababisha hali mbaya za kifedha na kiuchumi sambamba na kuibua matatizo ya kiusalama nchini.

Ayatullah Khamenei aliashiria pia masuala yaliyojitokeza hivi karibuni katika soko la fedha za kigeni na kuongeza kuwa: Tunapoyatazama mambo hayo kwa jicho la umakini tunashuhudia kuwepo mkono wa nchi ajinabi na mashirika yao ya kijasusi. 

Vita laini vinavyoendeshwa na nchi za Magharibi dhidi ya Iran

Nukta kuu na muhimu kuhusiana na masuala hayo ni kuwepo mfungamano baina ya malengo katika vita hivi laini. Kabla ya hapo pia, Ayatullah Khamenei alivitaja vita hivi laini vya adui kuwa ni hatari zaidi kuliko vile vya kijeshi na kusisitiza kuwa: Vita vya leo hii si vita vya kijeshi kwa sababu wao hawaendeshi vita vya kijeshi na wanakosea iwapo watataka kuanzisha vita vya kijeshi.  

Hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ni wazi kuwa inabainisha udharura wa kuhisi na kuwa macho viongozi na wasomi khususan katika Wizara ya Usalama wa Taifa ya Iran mbele ya majukumu muhimu na nyeti yanayowakabili.   

Maoni