Apr 21, 2018 07:27 UTC
  • Russia: Mradi wa makombora wa Iran hauna uhusiano wowote na JCPOA

Balozi wa Russia mjini Tehran amesisitiza kuwa, mradi wa makombora wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na siasa za Tehran kuhusiana na eneo hili hazina uhusiano wowote na maafikiano ya nyuklia yanayojulikana kwa jina la JCPOA.

Levan Jagarian amesema hayo leo Jumamosi alipohojiwa na mwandishi wa Radio Tehran na huku akipinga msimamo wa rais wa Marekani, Donald Trump, wa kutaka maafikiano hayo yafanyiwe marekebisho amesema, Moscow imekuwa ikisisitiza mara kwa mara kwamba haiungi mkono kufanyiwa marekebisho yoyote yale maafikiano hayo.

Pande za maafikiano ya JCPOA ,Marekani imo kwenye maafikiano hayo ingawa hivi sasa inatia ulimi puani na kufanya njama za kuyavunja

 

Amesema, maafikiano ya JCPOA ni hati muhimu sana, iliyozingatia pande zote na kukubaliwa na wote hivyo Russia haikubaliani na matokeo ya mazungumzo yanayofanyika nyuma ya pazia katika baadhi ya miji mikuu ya nchi za Ulaya baina ya Marekani, Ujerumani, Ufaransa na Uingereza, kwani mazungumzo hayo yanafanyika bila ya kuzishirikisha Russia, China na Iran.

Balozi huyo wa Russia mjini Tehran ameelezea kusikitishwa kwake na njama zinazofanywa na Marekani dhidi ya maafikiano hayo muhimu sana ya nyuklia na kuongeza kuwa, vitendo kama hivi vya Marekani vinazusha swali kwamba: "Hivi inawezekana kweli kuwa na imani na serikali ya Marekani?"

Amesema, mashinikizo na vitisho vya Marekani, Ujerumani, Ufaransa na Uingereza dhidi ya Iran vitashindwa tu kwani Russia na China zimesema mara nyingi kwamba zitaendelea kuheshimu na kushikamana kikamilifu na maafikiano ya nyuklia ya JCPOA.

Tags

Maoni