Apr 22, 2018 06:38 UTC
  • Misingi ya

Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameelekea mjini New York Marekani kushikiri katika kikao cha viongozi wa ngazi za juu cha "Amani ya Kudumu." Kikao hicho ni fursa nzuri ya kutoa mitazamo kuhusiana na amani na usalama duniani.

Matukio ya hivi sasa ya kieneo na kimataifa yanaonesha kuwa, suala la "Amani ya Kudumu" linahitajia mikakati na uchunguzi wa kina kuhusu muundo na sababu za kutokea machafuko duniani. Ni kwa njia hiyo tu ndipo itaweza kufanikishwa misingi mitatu mikuu ya Umoja wa Mataifa yaani, usalama na amani, ustawi na haki za binadamu.

Hata hivyo hadi hivi sasa kuna swali hili ambalo halijapatiwa majibu nalo ni kwamba; je, kuendelea migogoro na kukosekana amani na utulivu katika maeneo tofauti duniani sababu yake ni kutoheshimiwa malengo na misingi iliyomo kwenye Hati ya Umoja wa Mataifa au ni kwamba changamoto hizo zinatokana na kukosekana nia njema na ubeberu wa madola ya kiistikbari ulimwenguni?

Profesa Immanuel Kant

 

Takriban karne tatu nyuma, Immanuel Kant, mwanafalsafa wa Kijerumani aliandika katika kitabu chake kinachozungumzia masharti ya kupatikana amani ya kudumu kwamba, kujizuia kutumia mabavu na kuacha kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine ni miongoni mwa masharti hayo.

Hivi sasa pia sehemu kubwa ya mizozo na migogoro ya kimataifa inatokana na siasa za kupenda vita za Marekani na madola mengine ya Magharibi. Kuzikalia kwa mabavu Afghanistan na Iraq na kuuunga mkono kila upande na kwa hali na mali utawala wa Kizayuni wa Israel unaoikalia kwa mabavu Quds tukufu ni sehemu ya siasa hizo za kupenda vita za mabeberu wa dunia. Kwa zaidi ya nusu karne sasa, utawala wa Kizayuni wa Israel unazikalia kwa mabavu ardhi za Palestina na umewafanya wakimbizi Wapalestina milioni tano. Kwa miaka mingi umeuzingira kila upande Ukanda wa Ghaza, umeufungia njia zote za kuingia na kutoka na mara kwa mara unawashambulia wakazi wa eneo hilo kwa ndege za kivita na vifaru. Vyote hivyo ni vielelezo vya uvurugaji wa amani unaofanywa na madola ya kibeberu yakiongozwa na Marekani.

Gaston Bouthoul, mtaalamu wa masuala ya kijamii wa zama hizi anatoa maana ya neno amani akisema: Amani ni hali ambayo inaliwezesha kundi fulani la wanadamu kusimamia lenyewe mustakbali wake.

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani

 

Kutotekelezwa mikataba ya kuangamiza silaha na kutofanikiwa juhudi za kimataifa za kufuta vitisho vinavyotokana na kuwepo silaha za maangamizi ya umati hasa za nyuklia, ni kikwazo kingine kikubwa katika juhudi za kuleta amani ya kudumu duniani. Ugaidi nao ni moja ya matishio makubwa ya usalama na amani ya kimataifa. Uzoefu mchungu wa miaka ya hivi karibuni unaonesha kwamba kuna baadhi ya tawala za kiimla zenye misimamo mikali za eneo hili zinauchukulia ugaidi kuwa silaha ya kufanikishia malengo yao.

Amma Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo inaangalia mambo kwa jicho la ubinadamu na kwa misingi ya dini tukufu ya Kiislamu inaamini kuwa, mzizi wa vita na mizozo kati ya wanadamu unatokana na baadhi ya watu kupenda kuwakandamiza wengine, kufanya ubeberu, unyanyasaji na kukanyaga haki za wengine na inaamini kuwa, amani ya kudumu haiwezi kupatikana iwapo madola ya kibeberu yataendelea kukandamiza na kupuuza haki za mataifa mengine. Pendekezo la "Dunia iliyo dhidi ya machafuko na misimamo mikali" lililotolewa na Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kikao cha 68 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kupokewa vizuri na pia kupashiwa na baraza hilo ni ushahidi wa wazi wa imani hiyo ya Iran kwa kadhia ya "Usalama wa Kudumu."

Maoni