Mei 18, 2018 18:24 UTC
  • Mtazamo wa Kiongozi Muadhamu: Ukombozi usioepukika wa Palestina, kushindwa kusikokwepeka kwa Marekani + Picha

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, Baytul Muqaddas ndio mji mkuu wa Palestina na kwa taufiki na uwezo wa Mwenyezi Mungu Palestina itakombolewa tu kutoka katika makucha ya maadui na kwamba Marekani na vitimbakwiri vyake hawawezi kufanya upuuzi wowote mbele ya uhakika na sunna hiyo ya Mwenyezi Mungu.

Ayatullah Khamenei alisema hayo jana Alkhamisi katika mahafali yaliyojaa nuru ya kuwa na ukuruba na Qur'ani Tukufu na kusisitiza kuwa, matatizo yaliyopo hivi sasa katika ulimwengu wa Kiislamu ikiwemo hali ya kusikitisha ya Palestina na jinai za utawala wa Kizayuni hususan katika siku za hivi karibuni, ni matunda ya kujiweka mbali umma wa Kiislamu na mafundisho ya Qur'ani Tukufu. Aidha amesema, Marekani na nchi nyingi za barani Ulaya ni washiriki wa uhalifu na jinai zinazofanywa na Wazayuni. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile amesema: Umma wa Kiislamu,  madola ya Kiislamu na serikali za nchi za Waislamu zinapaswa kuchukua msimamo wa kukabiliana na jinai za Wazayuni. 

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamyu katika mahafali ya kuwa na mapenzi na ukuruba na Qur'ani Tukufu

 

Suala la Palestina ni nukta inayoukutanisha umma na madola ya Kiislamu na kwamba kulizingatia suala hilo na kuwa na hisia kali juu yake ni siasa za kimsingi za nchi za Kiislamu. Tab'an hapo katikati pana uzembe unaofanywa na baadhi ya nchi za Kiislamu, uzembe ambao daima umekuwa ukiwarahisishia njia Wazayuni ya kuzidi kudhihirisha sura yake halisi ya kigaidi. Maadhimisho ya mwaka wa 70 wa "Siku ya Nakba" ya kutangazwa rasmi kuundwa dondandugu la kensa katika kitovu cha ulimwengu wa Kiislamu yaani utawala wa Kizayuni wa Israel, yalionesha upeo wa juu zaidi wa jinai na uhayawani wa Wazayuni dhidi ya wananchi wasio na hatia wa Palestina. Kiburi hicho cha Wazayuni kisingelishuhudiwa kama si baadhi ya duru za Kiarabu kuingia katika mazungumzo ya mapatano yasiyo na natija na Wazayuni kwa uungaji mkono wa Marekani. Uungaji mkono wa kisiasa wa Marekani kwa utawala mtenda jinai wa Israel na wakati huo huo kuhisi utawala wa Kizayuni kuwa hakuna baya lolote litakaloukumba katika eneo hili, ni mambo ambayo yalizidisha kiburi cha Wazayuni hao cha kufanya jinai nyingine za kutisha siku ya Jumatatu sambamba na maadhimisho ya miaka 70 ya kuundwa utawala huo pandikizi. Wazayuni makatili waliwaua shahidi  na kwa umati Wapalestina 63 na kuwajeruhi wengine zaidi ya 2000 siku hiyo ya Jumatatu ya tarehe 14 Mei 2018 iliyosadifiana na kuhamishwa ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv na kupelekwa Baytul Muqaddas. Weledi wa mambo wanasema, hayo ndiyo matunda ya pembe tatu za shari zinazofanya mazungumzo ya mapatano yaani Marekani, Israel na baadhi ya duru za Kiarabu.

Sale al Na'ami, mtaalamu wa masuala ya kisiasa ameandika katika gazeti la al Arabi al Jadid la nchini Qatar kwamba: Hatua ya Marekani ya kuficha kimataifa vitendo viovu vya utawala vamizi wa Kizayuni imepelekea utawala huo kutopata hasara kubwa ya kisiasa kutokana na uvunjaji wake wa wazi wa haki za binadamu na kuwakandamiza waandamanaji wa Palestina. Mazingira yaliyopo hivi sasa katika eneo hili nayo yametoa mwanya kwa Israel kutumia wanajeshi wake kufanya jinai dhidi ya waandamanaji wa Palestina bila ya woga wowote.

Maandamano ya ukombozi wa Palestina yanawashirikisha watu wa matabaka yote na risasi na jinai za Israel haziwezi kuzima mwamko huu wa kupigiwa mfano

 

Hata hivyo, kulazinika utawala wa Kizayuni kutumia nguvu za kijeshi dhidi ya watu wasio na silaha wala ulinzi wanaoshiriki katika maandamano ya haki ya kurejea huko Palestina yanayofanyika kila Ijumaa katika mpaka wa Ukanda wa Ghaza na ardhi nyingine za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, kumezidi kuthibitisha wajibu wa kuendelea Wapalestina na muqawama wao na jinsi muqawama huo unavyozidi kupata nguvu licha ya kuweko uungaji mkono wa kila upande wa Marekani na vibaraka wake kwa utawala dhalimu wa Israel. 

Kiujumla ni kwamba, kukosekana umoja katika ulimwengu wa Kiislamu na kama alivyosema Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, kujiweka mbali Waislamu na mafundisho ya Qur'ani Tukufu ndizo sababu zilizoufanya utawala wa Kizayuni uendelee kufanya jinai dhidi ya Wapalestina. Lakini pia ni kama alivyosema Kiongozi Muadhamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei kuwa, kwa taufiki na uwezo wa Mwenyezi Mungu, Palestina itakombolewa tu kutoka katika makucha ya maadui na kwamba Marekani na vitimbakwiri vyake hawawezi kufanya upuuzi wowote mbele ya uhakika na sunna hiyo isiyoepukika ya Mwenyezi Mungu.

Hapa chini tumekuwekea baadhi ya picha zinazoonesha maandamano ya Wapalestina na jinsi taifa hilo madhulumu lilivyosimama kidete kupigania ukombozi wa haki zake.

Tags

Maoni