Mei 22, 2018 09:33 UTC
  • Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran yatoa jibu kwa matamshi machafu ya Pompeo

Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetoa taarifa maalumu inayoeleza kwamba matamshi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani dhidi ya Iran ni ishara ya kuemewa na kuishiwa nchi hiyo na kutojua la kufanya.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa: Iran inakanusha tuhuma za kile kilichoitwa stratejia mpya ya Marekani dhidi ya Iran; na matamshi ya Mike Pompeo ni uingiliaji wa wazi wa masuala yake ya ndani.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imefafanua kupitia taarifa hiyo kuwa matamshi machafu, ya matusi na ya uingiliaji masuala ya Iran ya Pompeo yaliyochanganyika na tuhuma zisizostahiki dhidi ya taifa kubwa na lililostaarabika la Iran ni ishara ya kuemewa na kuishiwa serikali ya Marekani katika kukabiliana na taifa la Iran huku ikitapatapa na kujaribu bila mafanikio kuzihadaa fikra za walimwengu kuhusiana na hatua iliyochukua ya kuvunja sheria na kukiuka makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imebainisha kuwa matamshi ya Pompeo yamedhihirisha kwa mara nyengine tena ufukara wa taarifa, udhaifu wa uono, utaahira wa kuhakiki mambo na mkanganyo uliopo katika mchakato wa upangaji na uchukuaji maamuzi ndani ya Marekani; na kuongeza kuwa mrengo wenye misimamo ya kufurutu mpaka na unaoshupalia vita unaotawala nchini Marekani hauifahamu wala hauwezi kujifunza kutokana na historia.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imebainisha katika taarifa yake hiyo kwamba licha ya upinzani wa nchi zote duniani ukiondoa tawala chache dhalili, utawala wa Marekani ambao umekiuka ahadi zote ulizotoa za kisiasa, kisheria na kimataifa, hauna ustahiki wala uwezo wa kuiwekea nchi kubwa kama Iran masharti ya eti kuheshimu ahadi ilizotoa.

Katika hotuba iliyojaa tuhuma zisizo na msingi dhidi ya Iran, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo jana alitangaza kile alichokiita stratejia mpya ya Washington ya kukabiliana na Iran baada ya nchi hiyo kujitoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.../

Tags

Maoni