Mei 22, 2018 10:32 UTC
  • Marekani; vikwazo dhidi ya Iran tangu mwanzo hadi hivi sasa (Kwa mnasaba wa kukumbuka mwaka Marekani ilipoanza kuiwekea vikwazo Iran)

Katika kipindi chote cha umri wa miaka 40 ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran, daima Marekani imekuwa ikifanya njama za kukwamisha maendeleo ya taifa la Iran. Vikwazo ni moja ya mbinu zinazotumiwa na Marekani kujaribu kufanikisha lengo lake hilo.

Tunapoangalia takwimu zinazohusiana na vikwazo tutaona kuwa Alkhamisi ya Mei 22, 1980, ilisadifiana na siku ya kwanza ya kuanza rasmi vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran

Mwaka 1980 Marekani iliweka vikwazo vikubwa dhidi ya Iran baada ya kutekwa pango lake la kijasusi (uliokuwa ubalozi wa Marekani) mjini Tehran na siku hiyo ya Alkhamisi ya Tarehe 22 Mei Washington ikaweka rasmi vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Iran. Mwaka 1995, Bill Clinton, rais wa wakati huo wa Marekani aliongeza vikwazo hivyo kwa kuyapiga marufuku mashirika ya mafuta ya Marekani kuwekeza katika sekta ya mafuta na gesi ya Iran. Vile vile uhusiano wa kibiashara wa Marekani na Iran ulivunjwa kwa mujibu wa mpango wa Damato na sheria ya ILSA. Kuanzia mwaka 2001 vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran ulikuja kwa sura mbili mapya katika uga wa kisiasa. Sura ya kwanza ilikuwa ni kuwawekea vikwazo vya kiuchumi watu na mashirika yasiyo ya kiserikali na ya pili ilikuwa ni kupanua wigo wa 'vikwazo erevu.'

Vikwazo

 

Marekani ilitangaza malengo kadhaa ya kuweka vikwazo hivyo vipya na miongoni mwake ni: kuzuia kuvunjwa haki za binadamu; kupambana na ugaidi, kuzuia kuenea silaha za nyuklia; kulindwa mazingira na kuzuia kuenea mizozo na vitisho katika eneo hili.

Kichekezo kikubwa ni kwamba, Marekani ndiye mtuhumiwa nambari moja wa kutoheshimu mambo yote hayo, kuanzia kupuuza kwake kulinda mazingira hadi kutojali kwake sheria za kimataifa zinazopiga marufuku kuzalisha na kueneza silaha za nyuklia, kuunga mkono ugaidi na kuvunja haki za binadamu. Hivyo kabla ya Marekani kuzituhumu nchi nyingine na kuyawekea vikwazo mataifa mengine, inabidi yenyewe iwajibu walimwengu kwa nini haiheshimu sheria hata moja kati ya hizo. 

Mashinikizo na uchochezi wa Marekani ulililazimisha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lipasishe vikwazo kadhaa vipya dhidi ya mradi wa nyuklia wa Iran. Hata hivyo mchezo huo wa kuigiza ulisimamishwa baada ya kufikiwa mapatano ya nyuklia ya JCPOA na kupasishwa azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa tarehe 20 Julai 2015. Pamoja na hayo, mapatano hayo ya nyuklia yenye baraka zote za jamii ya kimataifa, hayakupitisha hata miaka miwili kabla ya Marekani kutia ulimi puani na kujitoa katika mapatano hayo kwa madai ya kukabiliana na uwezo wa makombora wa Iran na ushawishi wa Tehran katika eneo la Mashariki ya Kati. Sambamba na hilo, serikali ya Donald Trump huko Marekani imepata kisingizio cha kuiwekea vikwazo vipya Iran. Katika kipindi chote hicho Marekani imekuwa ikisema kuwa inaweka vikwazo vya kulifanya kilema taifa la Iran. Hata hivyo hadi leo hii Washington imeshindwa kuagua ndoto na njozi zake hizo za alinacha.

Mwanafikra raia wa Marekani, Noam Chomsky

 

Noam Chomsky mwanafikra wa Kimarekani amenukuliwa akisema katika moja ya mahojiano aliyofanyiwa kwamba: Trump anachukua hatua za kudhoofisha nguvu za Marekani... Sijui iwapo anafanya hivyo kwa makusudi au kwa kutojua, lakini lengo lake kuu ni kutaka muda wote atangazwe na vyombo vya habari na kuzingatiwa na watu. Mtu analazimika kufanya mambo ya kipunguani kwa ajili ya kuhakikisha hatoki kwenye midomo ya watu na ya vyombo vya habari na ndio maana tunamuona Trump kila siku anafanya mambo ya kiwendawazimu.

Kwa kweli uanagenzi wa Trump unaonesha kuwa halijui vizuri taifa la Iran. Katika wakati wa utawala Barack Obama ambapo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema kuwa rais huyo wa Marekani anaficha makucha yake nyuma ya pazia, Washington ilitangaza wazi kuwa ina nia ya kuleta mabadiliko ya utawala nchini Iran, lakini Jamhuri ya Kiislamu imezidi kuwa imara. Hivyo ni jambo lisilo na shaka hata kidogo kwamba vitisho vya maneno vya Trump dhidi ya Iran navyo havina hatima nyingine ila kufeli tu kama ilivyojiri kwa njama na uadui wote wa huko nyuma wa Marekani dhidi ya Iran.

Maoni