Mei 24, 2018 08:12 UTC
  • Onyo la Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran kwa Ulaya kuhusu JCPOA

Admeri Ali Shamkhani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesema kuwa iwapo Ulaya itashindwa kutekeleza ahadi zake au kutumia vibaya hatua ya Marekani ya kujiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kwa ajili ya kuishinikiza Iran katika masuala mengine, basi bila shaka Tehran itaangalia upya siasa zake za kigeni.

Onyo la Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran kuhusiana na misimamo ya Ulaya na hasa baada ya kutolewa tetesi kadhaa kuhusiana na makubaliano hayo, ni sisitizo la mistari miekundu ambayo imewekwa wazi na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran bila kuzingatia masuala ya kisiasa, ili kuendelea kubakia katika mapatano hayo yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA). Hivi sasa kuna hatma mbili zinazoweza kuyakabili makubaliano hayo.

Mapatano ya nyuklia ya kimataifa JCPOA yaliyokiukwa na Marekani

Mosi ni kuendele makubaliano hayo ya nyuklia katika fremu ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kudhaminiwa maslahi yanayotokana nayo kwa Iran bila kuingizwa humo masuala mengine ya pembeni yasiyohusiana na makubaliano hayo yanayoendelea kati ya Iran na Umoja wa Ulaya. Jambo hilo linahitajia uhuru wa kivitendo, kisiasa na kiuchumi kutoka upande wa Ulaya kwa ajili ya kufungamana kikamilifu na makubaliano hayo. Uwezekano wa pili ni Umoja wa Ulaya kushindwa kutekeleza ahadi zake kuhusiana na makubaliano hayo mkabala na mashinikizo ya Marekani au kutumia vibaya hali mpya iliyojitokeza kwenye mapatano hayo, suala ambalo limewekwa wazi pia katika onyo la Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran.

Vitisho bandia vya Pompeo Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani dhidi ya Iran

Kwa mtazamo wa weledi wa mambo, makubaliano ya nyuklia ya JCPOA bila kuwepo Marekani yanakabiliwa na hali mbili zilizoashiriwa. Hali hiyo mpya ina mfungamano wa kisiasa na kiuchumi sambamba na kuheshimiwa haki ya kisheria ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kupitia maamuzi ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA, ambao ni msimamizi pekee wa kimataifa wa miradi ya nyuklia ya amani ya taifa hili. Katika uwanja huo Ali Shamkhani sambamba na kuashiria kutambuliwa rasmi urutubishaji wa urani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa unaofanyika kwa mujibu wa azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa amesema: "Namna ya kuendelea miradi ya nyuklia ya Iran kama ilivyoainishwa na makubaliano ya kimataifa ya JCPOA ni faili lililokwishafungwa, hivyo hakuna mazingira yoyote yatakayosababisha kufunguliwa tena faili hilo." Mwisho wa kunukuu.

Ulaya ina njia mbili, ima iheshimu mapatano hayo na kushirikiana kibiashara na Iran au kinyume chake

Kwa upande wa kisiasa, visingizio vilivyotolewa na Marekani kwa ajili ya kujiondoa katika makubaliano hayo na ambavyo vilikaririwa katika matamshi ya kipumbavu ya Trump na Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani dhidi ya Iran, ni tuhuma za kubuniwa na zisizo na ukweli wowote. Ama kuhusiana na nafasi ya Iran katika eneo la Mashariki ya Kati na kadhalika uwezo wa kiulinzi wa makombora yake ni kwamba, Jumatatu iliyopita Pompeo alitoa matamshi yaliyojaa tuhuma zisizo na ukweli wowote dhidi ya serikali ya Tehran. Alisema baada ya nchi yake kujiondoa katika makubaliano hayo, sasa inakusudia kuiwekea Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mashinikizo ya kifedha na vikwazo vikali mno ambavyo havijawahi kushuhudiwa huko nyuma, ili eti kuzuia upenyaji wa nchi hii kieneo na vilevile kuzuia kabisa miradi yake ya nyuklia na makombora.

Iran kwa Trump imemuwia sawa na mwiba uliomkwama kooni

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imetoa taarifa ambapo sambamba na kuashiria matamshi ya kijinga, yasiyo na thamani, ya udhalilishaji na ya uingiliaji ya Pompeo imesema: "Serikali ya Marekani ambayo licha ya kuwepo upinzani wa nchi zote za dunia isipokuwa tawala chache dhalili, imeamua kukiuka mikataba yote ya kisiasa, kisheria na kimataifa, haifai kuiainishia masharti nchi kubwa kama Iran ambayo imefungamana na ahadi zake." Mwisho wa kunukuu. Hivyo indhari ya Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran kuhusiana na mienendo ya Ulaya, imetolewa kwa mtazamo huo. Hasa kwa kuzingatia kuwa katika anga ya hivi sasa ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, kuna uwezekano mkubwa wa kujikariri ndani ya Umoja wa Ulaya yale yaliyofanywa na Marekani.

Maoni