Mei 28, 2018 11:36 UTC
  • Hatua kwa hatua kuelekea Siku ya Kimataifa ya Quds; Palestina imeanzia Mto Jordan hadi Bahari ya Sham!

Palestina ni suala kuu na la kwanza la Ulimwengu wa Kiislamu; na kufanyika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds katika Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kunatilia mkazo suala hilo muhimu na la kihistoria.

Imam Khomeini (Allah Amrehemu), mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambaye alikuwa na uelewa wa utambulisho halisi wa Israel na malengo ya Marekani katika eneo hili aliitangaza Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kuwa Siku ya Quds ili Waislamu duniani wazidi kuonyesha mshikamano kwa ndugu zao wa Palestina.

Kiongozi huyo mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliizungumzia Siku ya Quds kwa kusema:

Imam Khomeini (Allah Amrehemu) mwasisi wa Siku ya Kimataifa ya Quds

"Siku ya Quds si siku ya Palestina tu, ni siku ya kuyafahamisha pia madola makubwa kwamba hayawezi tena kusonga mbele ndani ya ardhi za Kiislamu.

Siku ya Quds ni siku inayopasa tutoe onyo kwa madola yote makubwa kwamba Uislamu hautakuwa tena chini ya udhibiti wenu, kupitia vibaraka wenu makhabithi; Siku ya Quds ni siku ya uhai wa Uislamu."

Hadi sasa taifa la Palestina limeshajitoa mhanga kwa mengi mno ili kulinda ardhi yake na kukabiliana na Wazayuni maghasibu; na licha ya mashinikizo yote yanayolikabili, lingali liko ngangari na limesimama imara. Hivi sasa hatima ya Palestina imefikia kwenye marhala nyeti na awamu hasasi. Nyangarika lililokubuhu kwa ushenzi na jinai liitwalo Israel, lililo mithili ya zimwi lenye uchu usiokwisha limeimeza sehemu kubwa ya ardhi ya Kiislamu ya Palestina; na kwa msaada wa Marekani linaendelea kutekeleza njama yake chafu katika Quds tukufu ili kukamilisha ughasibu wake wa ardhi hiyo.

Wananchi Waislamu wa Iran hushiriki kwa mamilioni katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds

Awamu mpya ya mauaji ya raia wa Palestina katika Ukanda wa Gaza hususan wanawake na watoto ni mwendelezo wa mbinu ileile ya utendaji jinai ambayo utawala wa Kizayuni wa Israel umeitumia katika miongo saba iliyopita dhidi ya Wapalestina.

Kwa mujibu wa Hati ya Umoja wa Mataifa, taifa lolote ambalo ardhi yake imevamiwa na kughusubiwa lina haki ya kujihami na kukabiliana na mvamizi kwa mtutu wa bunduki.

Khalid Qadumi, mwakilishi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS hapa nchini Iran anaizungumzia nukta hiyo kwa kusema:

"Ikiwa itahitajika, Muqawama utatumia silaha kukabiliana na utawala wa Kizayuni, na utatumia uwezo wake wote kupamana na adui; na kama itahitajika pia utafuatilia haki zake kwa maandamano ya amani."

Rais Hassan Rouhani katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds

Licha ya upinzani mkubwa kieneo na kimataifa, tarehe 14 Mei, serikali ya Marekani iliuhamishia mji wa Quds ubalozi wake uliokuweko Tel Aviv.

Sambamba na kufunguliwa ubalozi huo katika mji wa Baitul Muqaddas unaokaliwa kwa mabavu, Wapalestina wa Ukanda wa Gaza walifanya maandamano yaliyogeuzwa bwawa la damu baada ya kuzimwa kwa mkono wa chuma na askari katili wa utawala dhalimu wa Kizayuni. Wapalestina zaidi ya 60 waliuliwa shahidi na maelfu ya wengine walijeruhiwa katika ukandamizaji huo.

Siku ya Quds huadhimishwa na watetezi wa uhuru kote duniani

Hassan Rivaran, mtaalamu wa masuala ya Mashariki ya Kati anachambua chimbuko la jinai hizo kwa kuashiria dhati na utambulisho halisi wa utawala haramu wa Israel na kueleza kwamba:

"…Kwa kutegemea mapokeo bandia ya historia, kwamba kuna wakati Mayahudi waliwahi kuwepo katika ardhi ya Palestina, Wazayuni wanajenga hoja kuwa ardhi hiyo ni milki yao. Kama hiyo ni hoja, kwamba ikiwa taifa au kaumu ya watu waliwahi kuishi katika mahali fulani, mahali hapo patakuwa ni milki yao milele, itapasa tuseme kuwa sisi Wairani pia tuliwahi kuwepo Ugiriki na Misri na mwahali mwingine mwingi… Masuala yote haya ambayo wanayazungumzia hivi sasa kujipatia uhalali, hakuna hata moja kati yao yanayowapa uhalali huo."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Khamenei 

Mnamo mwezi Januari mwaka huu, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyed Ali Khamenei alihutubia hadhara ya washiriki wa mkutano wa 13 wa umoja wa mabunge ya nchi wanchama wa Jumuiya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) uliofanyika hapa mjini Tehran. Katika sehemu moja ya hotuba yake, Ayatullah Khamenei alisisitiza kwa kusema: "Bila shaka yoyote Palestina ni majimui na historia "inayoanzia Bahari ya Sham hadi Mto Jordan" na Quds nayo ni mji mkuu wake, na hakuna uwezekano wowote wa kupotosha ukweli huu."

Hakuna shaka kuwa suala la Palestina na kukaliwa kwa mabavu Quds tukufu ni moja ya migogoro mikubwa zaidi na ya wazi zaidi Magharibi ya Asia tangu nusu karne iliyopita hadi hivi sasa. Iran imekuwa kila mara ikiunga mkono kwa fahari na kutetea haki za taifa madhulumu la Palestina, na katika kipindi hiki nyeti haitasita hata chembe kuendeleza uungaji mkono wake huo…/  

     

 

Tags

Maoni