• Mkuu wa Kituo cha Kiislamu UK: Kwa mtazamo wa Imam Khomeini, Qur'ani imeleta ujumbe wa umoja

Mkuu wa Kituo cha Kiislamu nchini Uingereza ameashiria Wasia wa Kimaanawi na Kisiasa wa Imam Khomeini MA, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kueleza kwamba, kwa mtazamo wa kiongozi huyo Qur'ani imeleta ujumbe wa amani na umoja kwa jamii ya wanadamu.

Dakta Mohammad Ali Shomali ameyasema hayo katika maadhimisho ya mwaka wa 29 wa kukumbuka siku aliyoaga dunia Imam Khomeini (Allah Amrehemu) yaliyofanyika jana usiku katika kituo hicho mjini London, sambamba na kukaribia pia maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds.

Katika hotuba aliyotoa kwenye maadhimisho hayo, Dakta Shomali amezungumzia umuhimu wa Qur'ani kwa mtazamo wa mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kubainisha kuwa Imam Khomeini alikuwa akiwataka watu warejee kwenye Qur'ani na kuifanya kuwa ndio dira ya maisha yao.

Imam Khomeini MA, mwanzilishi wa Siku ya Kimataifa ya Quds

Mkuu wa Kituo cha Kiislamu cha Uingereza  ameongeza kuwa kwa mtazamo wa Imam Khomeini (MA) Qur'ani yenyewe ni rehma kubwa kabisa ya Allah.

Katika hafla hiyo, wazungumzaji wengine walizungumzia nukta mbalimbali kuhusu shakhsia ya Imam Khomeini (MA) na Siku ya Kimataifa ya Quds.

Maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds, iliyoasisiwa na Imam Khomeini, ambayo hufanyika kila mwaka katika Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani yatafanyika pia katika mji mkuu wa Uingereza, London. Maandamano hayo yanaandaliwa na kusimamiwa na Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Kiislamu ya Uingereza.../

Tags

Jun 03, 2018 15:02 UTC
Maoni