Jun 19, 2018 07:00 UTC
  • Kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, SEPAH, Hossein Hamadani aliyeuawa shahidi wakati akitoa ushauri wa kijeshi nchini Syria
    Kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, SEPAH, Hossein Hamadani aliyeuawa shahidi wakati akitoa ushauri wa kijeshi nchini Syria

Kiwewe cha wakuu wa Marekani na wa utawala wa Kizayuni wa Israel kutokana na kuweko Iran nchini Syria hakuna siku kitapungua na ndio maana viongozi hao wanashindwa kuzizuia ndimi zao kuzungumzia suala hilo.

Mbali na jambo hilo kuonesha ni kiasi gani joto la roho limewakaba viongozi hao wa Marekani na Israel, lakini pia madola hayo ya kiistikbari yanautumia uwepo wa Iran huko Syria kama kisingizio cha kuendelea na ubeberu wao katika eneo hili. Kwa kweli Marekani, Israel pamoja na Saudi Arabia muda wote zinahitajia kisingizio cha kuhalalishia ushirikiano wao wa kiistratijia wa kuendeleza siasa zao za kiistikbari katika eneo hili hata kama kisingizio hicho hakitaingilika akilini.

"McMaster" mshauri wa zamani wa usalama wa taifa wa rais wa Marekani Donald Trump alisema haya kuhusu 'hatari' ya Iran kwa Israel: Suala tunalokabiliana nalo hivi sasa, ni mkakati wa muda mrefu wa kuweko jeshi linalopigana kwa niaba ya Iran katika mipaka ya Israel

Uhusiano wa Iran na Syria hauishii tu baina ya serikali na serikali, bali umejikita pia katika nyoyo za wananchi

 

Naye Benjamin Netanyahu, waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni alisema katika mazungumzo yake na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa kwamba, Israel imebadilisha stratijia zake nchini Syria na inazihesabu harakati za Iran nchini humo kuwa shabaha ya mashambulizi yake.

Katika matamshi yake ya hivi karibuni kabisa ambayo yaliripotiwa siku ya Jumapili na gazeti la Kizayuni la Jerusalem Post, Netanyahu alisema: 

Sisi tutachukua hatua zozote zile kuzuia juhudi za kuutia nguvu (uwepo wa) kijeshi wa Iran na askari wanaopigana kwa niaba ya Iran karibu na mpaka (wa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu) hata kama itakuwa ni ndani ya ardhi ya Syria.

McMaster, mshauri wa zamani wa usalama wa taifa wa rais wa Marekani, Donald Trump

 

Matamshi hayo yanatolewa katika hali ambayo mara kwa mara viongozi wa Syria wamekuwa wakikanusha madai ya utawala wa Kizayuni yaliyo dhidi ya Iran na hata Iran nayo imeshasema mara chungu nzima kuwa, washauri wake wa kijeshi wako nchini Syria kwa mwaliko rasmi wa serikali ya nchi hiyo katika vita vyake dhidi ya magenge ya kigaidi.

Ijapokuwa kuangamizwa sehemu kubwa ya magenge ya kigaidi katika eneo hili kumetokana na taufiki ya Mwenyezi Mungu na jitihada kubwa za vikosi vya ulinzi na wananchi wanamapambano wa Iraq na Syria na kwa uungaji mkono wa pande zote wa Iran na Russia, lakini bado kuna safari ndefu hadi kung'oa kabisa mizizi ya magaidi hao na kurejeshwa utulivu na usalama wa kudumu katika eneo hili.

Kwa hakika, ili kuweza kuangamizwa kikamilifu ugaidi, kunahitajika kuweko welewa kamili kuhusu mambo yanayochochea ugaidi. Iran inayaelewa vyema mazingira nyeti ya hivi sasa na imeelekezea nguvu zake katika kukabiliana na changamoto zote zinazohatarisha usalama wa eneo hili ambapo dhihirisho la wazi zaidi la changamoto hizo ni magenge ya kigaidi. Msimamo huo wa Iran umezaa matunda mazuri kwa usalama wa kieneo na kimataifa. Hata hivyo viranja wa uovu katika eneo hili wanaounda muungano wa pembe tatu za shari, yaani Marekani, Israel na Saudi Arabia, hawafurahishwi hata chembe na mafanikio hayo ya Iran. Sababu yake ni kuwa, viranja hao wanatambua vyema kwamba, iwapo magaidi wataangamizwa kikamilifu, kutapatikana umoja na mshikamano katika ulimwengu wa Kiislamu, na wakati huo tena, mifumo ya kisiasa na kiusalama uliyobebeshwa ulimwengu wa Kiislamu haitakuwa na nafasi tena. Kwa kweli matamshi ya Benjamin Netanyahu ni dhihirisho la wazi la mbwa mwitu aliyejeruhiwa ambaye anahaha kila upande kurabirabi nafsi na kutafuta upenyo wa kubakia hai.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu (kushoto) na mfalme wa Saudi Arabia, Salman bin Abdulaziz

 

Katika kuonesha anayatambua vyema mambo yanayochochea vitendo vya ugaidi, Brigedia Jenerali Amir Hatami, Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu alisema katika hotuba yake kwenye kikao cha saba cha kimataifa cha usalama kilichofanyika mwezi Aprili mwaka huu mjini Moscow, Russia kwamba: Siasa za kimabavu na za kupenda kuhodhi kila kitu na kuuangalia usalama wa kimataifa kwa jicho la kulinda manufaa binafsi, kunaandaa uwanja bora kabisa wa kujitokeza na kukua vitendo vya kigaidi.

Tab'an kuna sababu nyingine nyingi zinazochangia jambo hilo. Mchezo unaofanywa na muungano wa kupambana na magaidi wa Daesh unaoongozwa na Marekani lakini kwa usimamizi wa Daesh yenyewe, kuunga mkono jinai za Israel huko Ghaza, kuhamishiwa Quds ubalozi wa Marekani uliokuweko Tel Aviv baada ya Donald Trump kuitangaza Quds kuwa eti ni mji mkuu wa utawala pandikizi wa Israel, kuendelea kuuliwa kinyama na kidhulma wananchi wa Yemen katika mashambulizi ya kikatili ya Saudi Arabia n.k, yote hayo ni tishio kubwa kwa usalama wa eneo hili na yanachochea kuweko misimamo mikali.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaamini kuwa, kushirikiana kikweli kweli katika kupambana na vitisho vya pamoja na kuleta utulivu na usalama wa kudumu katika eneo hili, kunahitajia kuweko siasa za kiulinzi za pamoja  na kupatikana mfumo wa kiusalama unaooana na mazingira ya bara la Asia unaotiwa nguvu na ushirikiano wa kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni ndani ya eneo hili bila ya uchochezi wa madola ajinabi.

Maoni