Jun 19, 2018 14:06 UTC
  • Maadui walijaribu kuizuia Iran kupata teknolojia ya kuunda injini za dizeli

Waziri wa Ulinzi wa Iran Brigedia Jenerali Amir Hatami ameshiriki katika sherehe ya uzinduzi wa injini ya dizeli iliyoundwa kikamilifu nchini Iran na kusema: "Injini hii ni kati ya teknolojia za kiviwanda ambazo adui alijaribu kuizuia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kupata kupitia vikwazo."

Injini hiyo yenye nguvu-farasi 1300 ilizinduliwa leo mjini Tehran katika sherehe iliyohudhuriwa pia na Waziri wa Ujenzi na Barabara, Waziri wa Viwanda na maafisa wa ngazi za juu wa kijeshi.

Katika hotuba yake, Brigedia Jenerali Hatami aliongeza kuwa, injini ya dizeli ni moja ya mahitajio muhimu ambayo yataiwezesha Iran kujitegemea. Ameongeza kuwa injini hiyo ya kitaifa ya dizeli imeundwa kwa kutegemea wataalamu, wasomi na wahandisi wa hapa nchini Iran. Amesema injini hiyo sasa itazalishwa kwa wingi nchini.

Akizungumza katika hafla hiyo, Sorena Sattari, Naibu Rais wa Iran anayeshughulikia masuala ya sayansi na teknolojia amesema uzinduzi huyo ni fahari kubwa kwa jamii ya teknolojia na wasomi Iran kwani hivi sasa uzalishaji wa injini ya dizeli umefikia kiwango cha kibiashara. Amesema katika siku za usoni Iran itazalisha kizazi kipya cha injini za dizeli.

Waziri wa Ulinzi wa Iran Brigedia Jenerali Amir Hatami 

Ikumbukwe kuwa mnamo Machi 20 mwaka 2018, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika ujumbe alioutuma kwa munasaba wa kuanza mwaka mpya wa Hijria Shamsia wa 1397 alisema adui hivi sasa anatumia vita vya kiuchumi kuilenga Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kwa msingi huo alisisitiza umuhimu wa kuunga mkono bidhaa za Kiirani. Aidha alisisitiza umuhimu wa kutegemea vipawa vya ndani ya nchi pasina kuwategemea ajinabi kama njia pekee ya kukabiliana na vita hivyo vya kiuchumi.

Maoni