Jun 23, 2018 07:21 UTC
  • Araqchi: JCPOA ipo katika ICU, yumkini Iran ikajiondoa wiki chache zijazo

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya kisiasa amesema makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na nchi sita za kundi la 5+1 maarufu kama JCPOA yako chumba cha wagonjwa mahututi ICU, na yumkini Tehran ikajiondoa kwenye mapatano hayo ndani ya wiki chache zijazo.

Abbas Araqchi ameyasema hayo katika kikao na waandishi wa habari mjini Vienna na kuongeza kuwa, nchi za Ulaya zinapaswa kujitoa muhanga kwa kuchukua hatua madhubuti na za maana ili kuyalinda makubaliano hayo.

Amesema JCPOA imepoteza mlingano wa asili baada ya Marekani kuchukua uamuzi wa upande mmoja na kujiondoa kwayo, na kwa msingi huo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inataka kuwekewa bayana dhamana ya kubakia hai mapatano hayo, kufikia mwishoni mwa mwezi.

Siku chache zilizopita, Rais Hassan Rouhani alisema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itajiondoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA iwapo itahisi haistafidi wala kupata maslahi yoyote kutokana na mapatano hayo ya kimataifa.

Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) 

 

Itakumbukwa kuwa Mei 8 mwaka huu, Rais wa Marekani, Donald Trump alitangaza kuindoa nchi yake kwenye mapatano ya JCPOA licha ya kwamba Washington ilikuwa mstari wa mbele kuyafanikisha wakati wa urais wa Barack Obama.

Nchi zingine tano zilizoafiki mapatano ya JCPOA, zikiwemo za Ulaya zimesisitiza kubakia katika mapatano hayo ya Vienna.

Tags

Maoni