Jun 23, 2018 13:53 UTC
  • ICJ kusikiliza kesi ya Iran dhidi ya Marekani kuhusu uzuiaji mabilioni ya dola

Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu (ICJ) imesema itasikiliza kesi iliyowasilishwa na Iran dhidi ya Marekani kuhusu mabilioni ya dola ya fedha za Iran ambazo serikali ya Marekani imezuzuia katika benki za nchi hiyo.

Katika taarifa, ICJ yenye makao yake The Hague Uholanzi imesema itaanza kusikiliza kesi hiyo ya mali za Iran kuanzia Oktoba 8 mwaka huu. ICJ, ambayo ni mahakama ya Umoja wa Mataifa imesema katika awamu ya kwanza itasikiliza pingamizi za Marekani kuhusu kesi hiyo.

Ikumbukwe kuwa Aprili 2016, Mahakama ya Kilele ya Marekani ilitoa hukumu na kusema dola bilioni mbili za Marekani ambazo zimezuiwa kwa muda mrefu nchini humo zinapaswa kukabidhiwa kwa familia za Wamarekani ambao waliuawa katika mlipuko wa bomu mwaka 1983 katika kituo cha kijeshi cha Marekani mjini Beirut na pia katika milipuko mingine. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif alitaja hatua ya mahakama moja ya Marekani kutoa hukumu ya kuchukua udhibiti wa dola bilioni mbili za Iran zinazozuiliwa nchini humo kuwa sawa na uharamia. Zarif alisema: "Huo ni wizi. Ni wizi mkubwa. Ni uharamia. Hakuna shaka tutachukua tena udhibiti wa fedha hizo."

Rais Hassan Rouhani wa Iran

Miezi miwili baadaye Iran iliwasilisha malalamiko rasmi ICJ kuhusu 'maamuzi yasiyo ya kisheria' katika mahakama za Marekani.

Rais Hassan Rouhani amesema serikali yake utafuatilia kesi hiyo hadi kuhakikisha kuwa taifa la Iran linapata haki zake na fedha hizo zinarejeshwa nchini na pia fidia inalipwa kwa hasara zilizopatikana.

 

Tags

Maoni