Jul 25, 2018 13:29 UTC
  • Rouhani: Umoja wa Wairani ni jibu imara kwa matamshi ya kipuuzi ya viongozi wa Marekani

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema vitisho hewa na visivyo na msingi vya baadhi ya viongozi wa Marekani havistahili kujibiwa na kueleza kuwa: Kutotetereka, kuwa na umoja na kutojali vitisho na njama za Marekani na kufanya juhudi za kuzisambaratisha njama za maadui, ndiyo jibu lenye nguvu zaidi la taifa la Iran kwa matamshi ya kipuuzi ya watawala wa Marekani.

Akizungumza leo Jumatano katika kikao na Baraza la Mawaziri hapa Tehran, Rais Hassan Rouhani ameashiria mashtaka yaliyowasilishwa na Iran katika Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu (ICJ) kuhusu hatua zilizochukuliwa na Marekani dhidi ya Iran na kueleza kuwa, akthari ya nchi duniani zimelaani na kuzitaja hatua hizo za Marekani kuwa si sahihi au kwa uchache zimeeleza kusikitishwa na hatua hizo.  

Rais Rouhani katika kikao na baraza lake la mawaziri 

Rais Rouhani pia amesema kuwa Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu (ICJ) ni chombo cha juu zaidi cha kisheria duniani na kusisitiza kuwa serikali ya Marekani inapasa kuwa na tahadhari mkabala na vitendo na mipango inayotekeleza kufuatia onyo lililotolewa na mahakama hiyo dhidi yake. 

Mahakama ya ICJ jana mchana ilitangaza siku ya kusikilizwa mashtaka yaliyowasilishwa na Iran dhidi ya Marekani na kuitaka serikali ya Washington ijiepusha kuchukua hatua yoyote mpya ya kurejesha vikwazo vya upande mmoja dhidi ya Iran.

Rais Donald Trump wa Marekani tarehe 8 mwezi Mei mwaka huu alikariri tuhuma zisizo na msingi dhidi ya Iran na kutangaza kujitoa Washington katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA sambamba na kuvirejesha vikwazo vya nyuklia dhidi ya Iran. 

Tags

Maoni