Aug 12, 2018 13:37 UTC
  • Rouhani na Putin wabadilishana mawazo kuhusu masuala ya kikanda na kimataifa

Marais wa Iran na Russia wamejadili na kubadilishana mawazo kuhusu masuala ya pande mbili, ya kikanda na kimataifa katika mazungumzo yao yaliyofanyika leo kandokando ya mkutano wa 5 wa viongozi wa nchi za pwani mwa Bahari ya Kaspi unaofanyika nchini Kazakshtan.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika katika mji wa bandarini wa Aktau, Rais Hassan Rouhani amesisitiza udharura na umuhimu wa kupanua zaidi uhusiano na ushirikiano wa Tehran na Moscow katika nyanja mbalimbali. 

Rais Rouhani amesema ushirikiano wa Iran na Russia katika Bahari ya Kaspi una manufaa kwa mataifa hayo mawili na kuongeza kuwa, bahari hiyo inapaswa kutambuliwa kuwa ni bahari ya amani na urafiki na sababu ya kuimarisha zaidi uhusiano, ushirikiano na urafiki baina ya nchi za kandokando yake. 

Rouhani amesema kuwa, ushirikiano wa pande mbili na pande kadhaa wa Iran na Russia katika masuala ya kikanda na kimataifa ikiwa ni pamoja na ushirikiano wa pande hizo mbili katika masuala ya usalama wa kieneo na katika kupambana na ugaidi wa kundi la Daesh huko Syria umekuwa na athari chanya na unapaswa kudumishwa hadi mizizi ya ugaidi itakapong'olewa kikamilifu. 

Kwa upande wake Rais Vladimir Putin wa Russia ameashiria uhusiano unaokua kila siku wa Russia na Iran katika nyanja mbalimbali na kusisitiza kuwa, Moscow iko tayari kustawisha zaidi uhusiano wake na Tehran katika masuala yote yenye maslahi kwa pande mbili. 

Rais Rouhani katika mkutano wa Aktau, Kazakhstan

Rais wa Russia amesema makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ni mkataba wa kimataifa wenye umuhimu mkubwa. Amesisitiza udharura wa kulindwa na kuimarishwa zaidi makubaliano ya nyuklia ya JCPOA baada ya Marekani kujiondoa katika makubaliano hayo na akasema kuna udharura wa kudumishwa mashauriano na ushirikiano kati ya Moscow na Tehran kwa ajili ya kupata utatuzi wa masuala mbalimbali ya kikanda na kimataifa.

Itakumbukwa kuwa Rais Rouhani mapema leo amehutubia mkutano wa Aktau nchini Kazakhstan ambako marais wa nchi tano za kandokando ya Bahari ya Kaspi wametia saini makubaliano ya mfumo wa kisheria wa bahari hiyo baada ya mazungumzo yaliyoendelea kwa kipindi cha miaka 21. 

Tags

Maoni