Aug 15, 2018 15:04 UTC
  • Rouhani: Adui ataingia nayo kaburini ndoto yake ya kuishinda Iran

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, shabaha ya vikwazo vya adui dhidi ya Iran ni kuwaweka katika matatizo wananchi wa taifa hili na kusisitiza kuwa, adui kamwe haiwezi kuishinda Iran bali njozi na ndoto yake hiyo atakwenda nayo kaburini.

Rais Rouhani amesema hayo leo (Jumatano) katika kikao cha Baraza la Mawaziri la Iran na kusisitiza kuwa, mshikamano wa wananchi wa Iran na viongozi wao hautomruhusu adui kufikia malengo yake. Amesema, adui hawezi kulifanyia upuuzi wowote taifa la Iran kwa vikwazo vyake haramu na visivyo na chembe ya huruma.

Iran: Vikwazo haviwezi kutulazimisha kubadilisha misimamo yetu

 

Amesisitiza kuwa, Iran inashirikiana na iko katika mazungumzo na nchi zote duniani na wakati huo huo amegusia pendekezo la Donald Trump la kutaka kufanya mazungumzo na Iran bila ya masharti yoyote na kusema kuwa, kutokana na vitendo ilivyofanya, Marekani imejiondolea uwezekano wowote wa kufanya mazungumzo na Iran.

Vile vile ameelezea kufurahishwa kwake na kuanza kurejea hali ya usalama katika eneo hili hususan Iraq, Syria, Lebanon na hata kaskazini mwa Afrika na kuongeza kuwa, hata Yemen nayo karibuni hivi itaishi katika usalama na utulivu kwani wavamizi wa nchi hiyo wameshapata funzo kuwa vita na uvamizi si jambo sahihi, bali njia sahihi ni mazungumzo, mapatano na maelewano. 

Tags

Maoni