Aug 20, 2018 08:15 UTC
  • Ujumbe wa Kiongozi wa Mapinduzi kwa Mahujaji: Sera za Marekani ni kuchochea vita na kuwaulisha Waislamu wenyewe kwa wenyewe

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema katika ujumbe wake kwa Mahujaji kwamba sera za Marekani ni kuchochea vita baina ya Waislamu na akasisitiza kwamba: inapasa kuzizima sera hizo za kishetani kwa umakini na kuwa macho na kwamba Hija na kujibari na washirikina vinawezesha kupatikana umakini huo.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema katika ujumbe uliotolewa leo kwa ajili ya Mahujaji wa Nyumba tukufu ya Allah kwamba kutengwa mahali maalumu pa kudumu kwa ajili ya faradhi ya Hija ni nembo ya kuleta umoja baina ya Waislamu na kujenga umma wa Kiislamu. Amefafanua kwamba: Hija katika mahali hapo na katika muda huu maalumu, kufanyika kila mara na miaka yote na kwa lugha ya kueleweka na ya mantiki iliyo wadhiha inawalingania Waislamu umoja; na hilo ni mkabala na takwa la maadui wa Uislamu ambao kila zama na hasa katika zama hizi wanawachochea Waislamu wakabiliane wenyewe kwa wenyewe.

Ayatullah Khamenei ameashiria mwenendo wa kiistikbari na wa utendaji jinai wa Marekani na kueleza kwamba: sera kuu ya Marekani katika kukabiliana na Uislamu na Waislamu ni kuchochea vita, kuwaulisha Waislamu wenyewe kwa wenyewe, kuwapa nguvu madhalimu dhidi ya wanaodhulumiwa, kuunga mkono mrengo wa madhalimu, kuwatumia kwa ajili ya kuwakandamiza kikatili wanaodhulumiwa na kuufanya kila mara mkali mno moto huo wa fitna inaouwasha.

Mahujaji wakiwa Arafa

Huku akiwataka Waislamu wawe macho na makini na kuzima siasa hizo za kishetani, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Hija inawezesha kuwa macho na kupatikana umakini huo na hiyo ndiyo falsafa ya kujibari na washirikina na waistikbari katika Hija.

Katika ujumbe wake huo kwa mahujaji, Ayatullah Khamenei ameongezea kwa kusema: Enyi mahujaji wapenzi! msisahau kuuombea dua umma wa Kiislamu na wanaodhulumiwa katika nchi za Syria, Palestina, Afghanistan, Yemen, Bahrain, Libya, Pakistan, Kashmir, Myanmar na maeneo mengineyo; na mwombeni Mwenyezi Mungu aikate mikono ya Marekani, waistikabri wengine na vibaraka wao.../

Tags

Maoni