Aug 23, 2018 01:40 UTC

Rais Hassan Rouhani amesema: "kujizatiti kulinzi Iran maana yake si kushupalia vita ila ni kutaka kuwa na usalama na amani endelevu, kwa sababu historia imetufunza kuwa kama hatutakuwa imara na wenye nguvu tutasambaratishwa."

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliyasema hayo siku ya Jumanne katika hafla ya uzinduzi wa ndege ya kivita iitwayo “Kowsar”, inayoruka kwa mwendo wa kasi kuliko ya sauti iliyoundwa kwa kutumia utaalamu wa ndani tu. Alibainisha kuwa: "ikiwa uwezo wa kiulinzi wa nchi hautawezesha kuzuia hujuma itakuwa sawa na kuzipa baraka na kuzitia tamaa nchi nyingine ya kuivamia nchi hiyo. Uwezo wa kuzuia hujuma maana yake ni kumfanya adui ahisi katika mahesabu yake kwamba endapo atajaribu kufanya uvamizi, nguvu na uwezo wa kiulinzi wa Iran utamhasiri na kumsababishia hasara kubwa mno."

Rais Hassan Rouhani akikagua maonyesho ya sekta ya ulinzi

Kwa kuwa nguvu na uwezo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran si tegemezi kwa nchi yoyote ile, leo hii katika mwaka huu wa 40 wa Mapinduzi ya Kiislamu, Iran inazidi kuwa na izza na heshima katika nyuga mbalimbali. Nguvu za kiulinzi, au kwa maneno mengine sekta ya ulinzi ndiyo, msingi wa uwezo wa kuzuia hujuma na uvamizi; na leo hii suala hili muhimu ndicho kipaumbele katika sera za ulinzi za Iran. Kadiri nchi yoyote ile inavyopunguza gharama za uwezo wake wa kiulinzi, kwa maana ya kutokuwa na utegemezi kwa yeyote yule, ndivyo inavyokuwa na kinga imara ya kukabiliana na vitisho vya aina yoyote ile. Pale nchi inapopanga mikakati ya uwezo wake wa kujihami na wa kuzuia hujuma kwa kutegemea suhula zake za ndani, adui hulazimika, kabla ya kuchukua hatua yoyote ile, kupanga mahesabu yake kwa kupima na kutathmini kwanza uwezo wa kiulinzi wa nchi hiyo. 

Kwa kuwa uwezo wa kiulinzi na wa kuzuia hujuma wa Iran umeratibiwa kwa kutegemea suhula na uwezo wa ndani umewanyima maadui fursa ya aina yoyote ile ya kuanzisha chokochoko kirahisi dhidi ya taifa hili. Kutokana na hali hiyo uwezo na nguvu za Iran zimeifanya Marekani, inayoimba kila mara wimbo wa kuanzisha vita, ifahamu kuwa kama itajaribu kuishambulia kijeshi Iran itadhurika na kupata hasara kubwa sana. Kuhusiana na nukta hiyo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei siku ya Jumatatu iliyopita alihutubia mkutano wa hadhara wa wananchi wa matabaka mbalimbali nchini, ambapo katika sehemu moja ya hotuba yake hiyo alizungumzia harakati za hivi karibuni za Marekani na kusisitiza kwa kusema: "hakuna vita vyovyote vitakavyotokea, kwa sababu kama ilivyokuwa huko nyuma, sisi katu hatutakuwa waanzishaji vita, na Marekani nayo pia haitaanzisha shambulio kwa sababu inajua kwamba watakaopata hasara kikamilifu ni wao, kwa sababu Jamhuri ya Kiislamu na wananchi wa Iran wamethibitisha kuwa watatoa kipigo kikubwa kwa mchokozi yeyote yule."

Amiri Jeshi wa vikosi vyote vya ulinzi, Ayatullah Khamenei akikagua gwaride la moja ya vikosi vya ulinzi

Ndege ya kivita ya “Kowsar” iliyozinduliwa siku ya Jumanne na kuanza kuruka kwa amri ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kielelezo cha kujitegemea katika uwezo wa kijeshi wa kuzuia hujuma yoyote ile ya adui. Ndege ya kivita ya Kauthar inayopaa kwa mwendo wa kasi zaidi kuliko wa sauti imeundwa kwa kutegemea utaalamu wa ndani tu wa hapa nchini Iran na hivyo kuongeza zaidi uwezo wa kuzuia hujuma na uvamizi; kwa sababu wataalamu wa kigeni hawakuwa na nafasi yoyote katika utengezaji wa ndege hiyo; na nukta hii muhimu imepunguza kiwango cha gharama za kiulinzi za Iran.

Waziri wa Ulinzi, Brigedia Jenerali Amir Hatami

Akihutubia hafla hiyo ya siku ya Jumanne ya maadhimisho ya Siku ya Sekta ya Ulinzi, Waziri wa Ulinzi wa Iran Brigedia Jenerali Amir Hatami alisisitiza kwa kusema: sekta ya ulinzi ni stratejia pana ya vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayodhamini na kulinda kujitawala na izza ya kitaifa na ni nembo ya kujiamini na kujitegemea taifa la Iran.../

Tags

Maoni