Aug 29, 2018 07:40 UTC
  • Kuulizwa Rais wa Iran maswali bungeni ni kielelezo cha demokrasia katika mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, jana Jumanne alifika katika Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge la Iran, kujibu maswali ya wabunge. Kwa mujibu wa kipingee cha 88 cha Katiba ya Iran; kumuuliza maswali rais wa nchi ni moja ya majukumu ya wabunge.

Kwa mujibu wa jukumu hilo na katika fremu ya katiba; Rais wa Jamhuri ya Kiislamu jana alifika bungeni kujibu maswali ya wabunge kuhusu hali ya kiuchumi nchini hasa kuhusu kutofanikiwa serikali katika kudhibiti ulanguzi wa bidhaa na fedha za kigeni, kuendelea vikwazo vya kigeni, kushindwa kupunguza ukosefu wa ajira, kudorora uchumi na kupanda thamani ya fedha za kigeni.

Udhaifu katika usimamizi wa sekta ya uchumi ni kati ya masuala ambayo hayana uhusiano wa moja kwa moja na Marekani kujiondoa katika mapatano ya nyuklia ya Iran yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji, JCPOA. Pamoja na hayo, baada ya Marekani kujiondoa katika JCPOA, hali mpya ya kiuchumi imeibuka nchini Iran. Lakini pia hakuna shaka kuwa kumekuwepo na udhaifu na mapungufu katika mipango ya kiuchumi ya serikali ya Rais Hassan Rouhani. Hatua ya bunge kuamua kufuatilia suala hilo kwa kumuita rais bungeni ajieleze haipaswi kutathminiwa kuwa ni kuwepo msuguano baina ya mihimili hiyo miwili ya dola.

Kama alivyosema Ali Larijani, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, kufika rais wa nchi katika bunge kunaonyesha kina cha demokrasia hapa Iran na ni fahari kwa taifa kuwa rais amefika bungeni ili kuwajibika mbele ya wananchi.

Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Sayyed Naqavi Husseini, mbunge na mwanachama wa Tume ya Usalama wa Taifa katika bunge na ambaye alikuwa miongoni mwa waliomuuliza rais maswali ameashiria kadhia hiyo ya kufika rais bungeni kujibu maswali ya wabunge na kusema suala hilo halina maana kuwa kuna uhasama baina ya bunge na serikali. Ameongeza kuwa: "Tunawatangazia maadui kuwa, tutaikanyaga Marekani na bunge linamuunga mkono Rais.

Rais Hassan Rouhani pia naye amesema siku hii ambayo amefika bungeni na kujibu maswali ya wabunge ni siku iliyojaa baraka kwa demokrasia nchini.

Mtazamo huo unaonyesha kuwepo uwezo mkubwa wa kidemokrasia katika mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na pia ni ishara ya uwajibikaji wa viongoni na katu si ishara ya udhaifu.

Hakuna shaka kuwa, serikali na bunge ni mihimili miwili inayojitegemea katika mfumo na kila moja una jukumu muhimu na majukumu hayo yanapaswa kutekelezwa kwa ushirikiano ili kufikia lengo la pamoja.

Uwajibikaji wa serikali katika nchi zenye kufuata mfumo wa demokrasia unaweza kuangaziwa kwa mitazamo mitatu.

Awali, ni kuhusu uwajibikaji kisheria. Ufahamu wa utawala wa kisheria kimsingi una maana ya kuwa mtu ambaye anatekeleza sheria na sera anapaswa kutenda kazi kwa mujibu wa vipimo vilivyokwa kisheria.

Pili ni kuhusu uwajibikaji wa serikali ukiwemo uwajibikaji wa kisiasa na nukta hii ina maana kuwa, serikali au watendaji wakuu wa nchi wanapaswa kuwajibika mbele ya bunge na wananchi kuhusu utendaji kazi wao.

Tatu ni kuwa, uwajibikaji wa serikali pia unajumuisha uwajibikaji wa kifedha. Nukta hii ina maana kuwa, wakuu wa serikali wanapaswa kuwajibika kuhusu namna wanavyotumia pato la nchi kwa mujibu wa sheria zilizopitishwa na bunge.

Maudhui ya maswali ya wabunge kwa Rais Rouhani yanaashiria kina cha fikra ya demokrasia katika mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ambapo wakuu wote wa nchi wanapaswa kuwajibika. Tunaweza kusema kuwa mfumo wa demokrasia kwa hakika umejengeka katika msingi wa sheria na haki ya wananchi na hivyo hakuna yeyote anayepaswa kukwepa kuwajibika.

Wabunge hawakuridhika na aghalabu ya majibu aliyotoa rais, na kwa mujibu wa sheria majibu manne ambayo hawakuridhika nayo yatatumwa kwa Idara ya Mahakama. Baada ya uchunguzi utakaofanywa katika idara ya mahakama, faili hilo litarejeshwa bungeni ili uamuzi wa mwisho uchukuliwe. Masuala ya kiuchumi na kimaisha nchini yana mitazamo miwili ya ndani na nje ya nchi. Kwa mtazamo wa nje ya nchi, matatizo hayo yanatokana na njama za Marekani katika fremu ya vikwazo ambavyo lengo lake ni kulipigisha magoti taifa la Iran. Kwa mtazamo wa ndani ya nchi, ni wazi kuwa kuna baadhi ya dosari ambazo zinapaswa kuzingatiwa. Kufanyika kikao hicho cha bunge jana cha wabunge kumuuliza rais maswali ni nukta inayoashiria ulazima wa kurekebisha dosari zilizopo nchini.

 

Tags

Maoni