Aug 30, 2018 02:19 UTC
  • Mwenendo

Inavyoonesha, hivi sasa viongozi wa Marekani wameamua kwa wakati mmoja kuendesha "vita vya kisaikolojia na kipropaganda" na "vitisho vya kijeshi" katika harakati zao wanazofanya kwenye eneo hili la Mashariki ya Kati.

Katika mwendelezo wa harakati hizo, Waziri wa Ulinzi wa Marekani James Mattis ametoa matamshi ya kifidhuli wakati wa safari yake nchini Afghanistan kwa kudai: "Sisi tumeionya Iran kutokana na mwenendo wake nchini Syria na Yemen na kwa kuwaunga mkono Wahouthi. Iran itawajibishwa kwa kila mwenendo wake "mbaya" katika eneo."

Waziri wa Ulinzi wa Marekani anaituhumu Iran na kudai kuwa inaingilia masuala ya nchi nyingine na ina mwenendo "mbaya" na haribifu, ilhali Jamhuri ya Kiislamu imetoa msaada wa kweli na wa dhati katika kuyaangamiza magaidi nchini Syria na Iraq. Na hii ni katika hali ambayo Marekani ina faili chafu kutokana na kuingilia masuala ya ndani ya Iran kuanzia tangu ilipohusika na mapinduzi ya kijeshi ya Mordad 28, 1332, yaani Agosti 19, 1953 na kuiangusha serikali halali ya Waziri Mkuu Mohammad Mosaddegh; kisha ilipousaidia na kuunga mkono utawala mtenda jinai wa Saddam katika vita vya miaka minane dhidi ya Iran, kuiangusha ndege ya abiria ya Iran sambamba na kuendeleza hatua za kiuadui na kihasama dhidi ya taifa hili kwa muda wa miongo minne sasa.

James Mattis, maarufu kama "Mbwa Kichaa"

Kitambo si kirefu nyuma gazeti la Washington Post linalochapishwa nchini Marekani liliandika makala ya kukosoa matamshi mengine ya kifidhuli yaliyotolewa na yeye Mattis mnamo mwezi uliopita wa Julai alipotaka utawala uliopo nchini Iran uondolewe. Katika makala hiyo, gazeti hilo liliandika: "Kupinduliwa Mosaddeqh na kuurejesha madarakani utawala wa kidikteta na kipenzi cha Magharibi kulizidi kuwafanya Wairani waamini kwamba Marekani na Uingereza ni mabeberu mamboleo na madhalimu wanaoingilia mambo ya ndani ya mataifa mengine." Eisenhower, rais wa 34 wa Marekani naye pia aliashiria kwenye kitabu cha kumbukumbu zake kuhusu tukio la tarehe 8 Oktoba 1953 na kuandika kuhusiana na mapinduzi hayo ya kijeshi kwamba: "Tulichokifanya kilikuwa siri. Lakini kama watu wote watakifahamu, hatutaona aibu katika eneo pekee...". 

Lakini badala ya viongozi wa Marekani kuona aibu kwa waliyoyafanya, wameamua kujisahaulisha historia na badala yake kuanzisha mchezo hatari, ambapo sambamba na kuzusha tuhuma dhidi ya Iran wanajaribu kupotosha ukweli halisi wa mambo. Badala ya kuituhumu Iran, viongozi wa Marekani wanapaswa kuyatolea majibu masuali mengi, ikiwa ni pamoja na kueleza, uvamizi wa Washington dhidi ya Afghanistan na Iraq ulifanywa kwa malengo gani, na kwa nini wanayaelekeza matukio ya Syria kwenye migogoro mingine mipya.

Marekani imeamua kufumbia macho ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa nchini Bahrain, ambayo imeigeuza kuwa kituo chake kikuu cha kijeshi. Kwa kujiingiza kijeshi Mashariki ya Kati, Marekani imesababisha hasara na madhara makubwa kwa amani na usalama wa eneo la Ghuba ya Uajemi; na haina kingine inachowaza zaidi ya kustawisha soko lake la uuzaji silaha kwa Saudi Arabia na nchi nyingine za Kiarabu za eneo hili.

Rais wa Marekani Donald Trump

Ukweli ni kwamba Marekani huwa kila mara inatafuta njia ya kujinufaisha kwa kutumia matatizo ya wengine. Hivi sasa ambapo eneo la Mashairiki ya Kati limekumbwa na taharuki ya vita dhidi ya ugaidi, Washington inalitumia pia suala hilo kuzusha chokochoko na fitna ya kueneza hofu na chuki dhidi ya Iran. Kutokana na matamshi ya Mattis ni dhahiri kwamba anachojaribu kufanya ni kuanzisha mada isiyohusu ili kugeuza mkondo wa kinachopasa kujadiliwa. Marekani ndiyo msababishaji halisi wa vita, ugaidi na wimbi la misimamo ya kufurutu mpaka lililozikumba nchi za eneo hili, ambalo chanzo chake kinarejea miaka kadhaa nyuma kwenye uingiliaji kijeshi uliofanywa na nchi hiyo katika eneo. Matokeo ya uingiliaji huo unashuhudiwa leo hii katika ugaidi na harakati zilizoratibiwa za misimamo ya kufurutu ada katika nchi za Afghanistan, Iraq, Syria na maeneo mengine duniani. Lakini viongozi wa Marekani wamezoea kuwatuhumu na kuwatupia mpira wengine na wakati huohuo kutumia lugha ya uongo na uzandiki ili kuhalalisha na kuonyesha kuwa lengo la hatua wanazochukua wao ni kuleta amani na usalama, wakati ukweli ni kwamba kutokana na rundo la mafaili ya jinai ilizotenda, uingiliaji wa kijeshi iliofanya, moto wa vita iliowasha pamoja na uvunjaji wa sheria za kimataifa na uwekaji wake wa vikwazo haramu, Marekani na viongozi wake ndio wanaopaswa kufuatiliwa na kuwajibishwa.../

 

 

Maoni