Aug 30, 2018 08:04 UTC
  • Hotuba ya Ayatullah Khamenei mbele ya Rais na Baraza  la Mawaziri; kibainishi cha njia ya kukabiliana na matatizo na njama za maadui

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Jumatano ya jana alikutana na Rais Hassan Rouhani pamoja na baraza lake la mawaziri na kusisitiza nukta kadhaa muhimu kuhusiana na masuala ya kiuchumi, sera za kigeni, umoja na mshikamano wa ndani hapa nchini.

Sehemu kubwa ya hotuba hiyo ya Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ilibainisha yanayopasa na yasiyopasa kufanywa katika sera za kigeni na namna ya kuyapatia ufumbuzi matatizo ya kiuchumi.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza juu ya udharura wa kuweko uhusiano mzuri na unaostawishwa zaidi na majirani na akasema kuhusiana na madola ya Ulaya kwamba: Hakuna tatizo kuwa na uhusiano na madola ya Ulaya na kuendeleza mazungumzo nayo, lakini sambamba na kuendelezwa hilo, hampaswi kuwa na matumaini na madola hayo kuhusiana na masula kama ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA au suala la uchumi.

Ukosoaji wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusiana na muamala usiofaa wa madola ya Ulaya katika masuala kama ya JCPOA na vikwazo ulikuwa wazi na bayana. Kama ambavyo kabla ya hapo pia Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alibainisha hilo, mara hii pia amesema wazi kabisa kwamba: Ahadi za madola ya Ulaya zinapaswa kutazamwa kwa jicho la shaka na kuwa makini juu ya mchakato mzima.

Baadhi ya mawaziri katika mkutano na Kiongozi Muadhamu

Ayatollah Khamenei ameyataja mapatano ya nyuklia ya JCPOA kuwa ni wenzo wa kuweza kulinda manufaa ya taifa na kuongeza kwamba, mapatano hayo si lengo, bali ni njia ya kufikia malengo na tukiona hayatulindii manufaa yetu ya kitaifa tutaachana nayo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia juu ya kutokuweko uwezekano wa kufanya mazungumzo na Wamarekani na kuongeza kuwa, natija ya mazungumzo na viongozi wa kabla wa Marekani ambao kwa uchache hawakuonyesha dhahiri hakika yao imekuwa hii, tutakuwa na mazungumzo gani na viongozi wa sasa waovu na wenye midomo michafu ambao wamefunga panga kiunoni kwa ajili ya kukabiliana na Wairan. Hivyo basi hakuna mazungumzo ya kiwango chochote kile yatakayofanyika baina ya Iran na Wamarekani.

Ayatullah Khamenei ameeleza kuwa, mazungumzo na Iran ni hitajio la serikali zote zilizoingia madarakani nchini Marekani na  kubainisha kwamba: Kikubwa kinachopiganiwa na serikali hizo za Marekani ni kutaka kuwaonesha walimwengu kuwa zimeweza kuivuta kwenye mazungumzo hata Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, lakini kama tulivyobainisha wazi na bayana na kwa hoja huko nyuma ni kwamba, hatutofanya mazungumzo yoyote yale na viongozi wa sasa wa Marekani.

Rais Rouhani na baraza lake la mawaziri katika Sala ya Jamaa iliyoongozwa na  Ayatullah Khamenei 

Hotuba ya Kiongozi Muadhamu imebainisha juu ya kushughulikia matatizo na wakati huo huo kuzingatia uwezo na kuwa makini katika siasa za kigeni. Katika kipindi cha miaka 40 iliyopita, Marekani imefanya kila uadui iliyoweza kuufanya dhidi ya mapinduzi, taifa na Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu. Hivi sasa matumaini yote ya Marekani yamekita katika kuleta mpasuko na hitilafu za ndani hapa nchini na kuilazimisha Iran isalimu amri mbele ya mashinikizo ya kiuchumi.

Ni kwa kutilia mkazo nukta hii ndipo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu akasisitiza juu ya udharura wa "kutumia uwezo mkubwa na mwingi wa kiuchumi". Ayatullah Khamenei ameashiria ripoti ya vituo vya kimataifa na kuongeza kuwa, kwa upande wa uwezo ambao bado haujatumiwa, Iran inashika nafasi ya kwanza duniani.

Kiongozi Muadhamu ameeleza kuwa: Kwa mujibu wa takwimu za taasisi za kimataifa, filihali Iran inashika nafasi ya 18 miongoni mwa nchi mia mbili katika uga wa uzalishaji mali ghafi za ndani, na endapo uwezo wa ndani utatumiwa zaidi na kwa njia bora, tunaweza kufikia katika daraja za juu zaidi duniani.

Mohammad Javad Azari Jahrami, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia za Mawasiliano  (wa kwanza kulia) akiandika nukta katika kikao cha Kiongozi Muadhamu na Rais Hassan Rouhani pamoja na baraza lake la mawaziri 29.08.02018

Kwa kuitupia jicho hotuba ya Kiongozi Muadhamu kwa mtazamo huo tunaweza kuona kwamba, imejikita katika nukta mbili muhimu. Mosi ni kuwa, katika kukabiliana na matatizo hakuna wakati ambao Iran ilichukua msimamo dhaifu, ililegeza kamba au kusalimu amri mbele ya mashinikizo. Nukta ya pili ni kwamba, Iran haijasahau tajiriba na uzoefu wa huko nyuma na inatambua vyema utambulisho halisi wa Marekani.

Katika kipindi hiki pia, taifa la Iran limesimama imara, madhubuti na kwa kujiamini kikamilifu mkabala na matatizo na njama mbalimbali na linafahamu vizuri kwamba, ufumbuzi wa matatizo haya ni kutegemea uwezo wake wa ndani wa nchi na sio kupitia ahadi tupu na zisizotekelezwa kivitendo za Ulaya na pande nyingine katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA. 

Maoni