Aug 31, 2018 13:06 UTC
  • Safari ya Zarif mjini Islamabad; kufunguliwa ukurasa mpya wa uhusiano wa Iran na Pakistan

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameelekea nchini Pakistan kwa safari rasmi ya siku mbili akiwa mwanadiplomasia wa mwanzo wa kigeni kutembelea nchi hiyo na kukutana kwa mazungumzo na maafisa mbalimbali wa serikali mpya chini ya uwaziri mkuu wa Imran Khan.

Mohammad Javad Zarif aliwasili mjini Islamabad jana Alkhamisi na katika mahojiano na waandishi wa habari alisema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina uhusiano mzuri na wa kihistoria na Pakistan. Baada ya mazungumzo na Asad Qaisar, Spika wa bunge la taifa la Pakistan, Zarif alisema Iran inataka kuwa na uhusiano bora na imara zaidi na Pakistan na kuongeza kwamba ana matumaini wakati wa serikali mpya ya nchi hiyo chini ya uwaziri mkuu wa Imran Khan uhusiano wa kirafiki wa nchi mbili utapanuka na kustawi zaidi.

Uhusiano wa Iran na Pakistan umekuwa ukipewa umuhimu siku zote na viongozi wa ngazi za juu wa nchi mbili kutokana na masuala ya pamoja ya pande hizo yakiwemo ya kidini, usalama wa pamoja wa mpakani na mapambano dhidi ya ugaidi.

Kustawisha uhusiano na majirani zake ni suala linalopewa kipaumbele katika sera za nje za Iran; na katika muktadha huo, Iran ina mtazamo maalumu kuhusiana na Pakistan. Hivi sasa serikali mpya imeingia madarakani nchini Pakistan, na kama ilivyo Iran, nayo pia ina mtazamo maalumu juu ya uhusiano wa nchi hizo mbili jirani; na hilo linahesabiwa kuwa nukta ya pamoja ya kistratejia kwa ajili ya kuanza awamu mpya katika uhusiano wa Iran na Pakistan. Suala hilo muhimu lilishuhudiwa kwa uwazi kabisa katika mazungumzo ya simu yaliyofanyika hivi karibuni kati ya Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Imran Khan, Waziri Mkuu mpya wa Pakistan. Katika mazungumzo hayo, Imran Khan alisema:"Nakuhakikishia kuwa uhusiano wa nchi mbili utastawi zaidi; na Pakistan inakupa umuhimu maalumu kustawisha uhusiano wake na Iran."

Rais Hassan Rouhani wa Iran (kulia) na Waziri Mkuu mpya wa Pakistan Imran Khan

Mbali na Iran na Pakistan kushirikiana katika masuala ya usalama na mapambano dhidi ya ugaidi suala ambalo limekuwa likifuatiliwa kila mara na maafisa wa pande mbili, kwa upande wa kiuchumi pia zinaweza kila moja kukidhi mahitaji ya mwenzake. Iran ina uwezo mzuri katika nyanja ya nishati na huduma za ufundi na uhandisi, kwa hivyo inaweza kukidhi mahitaji muhimu ya Pakistan katika sekta ya nishati hususan ya umeme. Bomba la kusafirisha gesi kutoka Iran kuelekea Pakistan, suala linalozungumziwa kwa miaka kadhaa sasa na nchi mbili, na ambalo ujenzi wake haukupiga hatua huko nyumba kutokana na baadhi ya sababu za kisiasa, limezungumziwa tena hivi sasa kwa uzito mkubwa katika kipindi hiki cha uwaziri mkuu wa Imran Khan. Muhammad Abdulbasit, msemaji wa zamani wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan analielezea suala hilo kwa kusema: Mazungumzo ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Waziri Mkuu mpya wa Pakistan yana umuhimu mkubwa sana. Kwa sababu Zarif na Imran Khan watachukua maamuzi mapya kuhusiana na kufufua bomba la usafirishaji gesi kati ya nchi mbili ili kwa njia hiyo suala la uhaba wa gesi na nishati nchini Pakistan liweze kutatuka.

Ushirikiano wa kiuchumi baina ya nchi mbili unapewa kipaumbele maalumu

Kwa kuzingatia kuwa hivi sasa viongozi wapya wa Pakistan wanaangalia upya sera za nchi hiyo kuhusiana na Marekani, awamu mpya ya uhusiano wa Iran na Pakistan inatoa mwanga wa matumaini; na hatua hiyo itadhamini manufaa na maslahi ya taifa ya nchi hizo mbili. Sera za Pakistan za kuwa na misimamo huru zaidi katika kipindi hiki cha uwaziri mkuu wa Imran Khan zitarahisisha mwenendo wa ushirikiano kati ya Tehran na Islamabad na matokeo yake ni kuzifanya Iran na Pakistan ziwe na mtazamo wa pamoja na wenye kukaribiana zaidi katika masuala yanayohusu uhusiano baina ya pande mbili na wa kieneo. Katika uga wa pande mbili, ushirikiano wa kiuchumi ukiwemo wa ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi kutoka Iran kuelekea Pakistan utashuhudia uchukuaji misimamo takriban ya aina moja; na mafanikio ya mradi huo muhimu yatakuwa na manufaa kwa nchi zote mbili jirani. Isitoshe, mapambano dhidi ya ugaidi ambao ni changamoto kali kwa eneo na kudhamini usalama katika mpaka wa pamoja ni masuala yanayoingiliana pamoja. Serikali mpya ya Pakistan inapinga tafsiri inayotolewa na Marekani juu ya kupambana na ugaidi; na inavyoonekana itafuata muelekeo huru na wa kujitegemea katika uga huo; suala ambalo litakuwa na taathira chanya katika awamu hii mpya ya uhusiano wa Iran na Pakistan.../ 

Tags

Maoni