Aug 31, 2018 13:55 UTC
  • Zarif: Hatuna mpaka wowote katika kustawisha uhusiano wetu na Pakistan

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Iran haina mpaka wowote katika kukuza na kustawisha uhusiano wake na jirani yake Pakistan.

Dakta Muhammad Javad Zarif amesema hayo leo mjini Islamabad katika mazungumzo yake na Shah Mehmood Qureshi Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Pakistan na kubainisha kwamba, nchi hiyo ni jirani muhimu wa Iran.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, hakuna nchi ya tatu ambayo inaweza kuwa na taathira hasi katika uhusiano wa Tehran na Islamabad. 

Dakta Zarif amesisitiza katika mazungumzo yake hayo juu ya udharura wa kustawishwa na kukuzwa zaidi uhuusiano wa nchi mbili hizo jirani katika nyanja mbalimbali kama za kudhamini usalama wa mpakani, ushirikiano wa kibandari, masoko ya mpakani, ushirikiano wa kibenki na kadhalika.

Dakta Muhammad Javad Zarif (kushoto) akiwa katika mazungumzo na Asad Qaiser, Spika wa Bunge la Pakistan 31.08.2018

Kabla ya mazungumzo yake na Shah Mehmood Qureshi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Pakistan, Dakta Zarif alikutana na kufanya mazungumzo pia na Qamar Javed Bajwa, Kamanda wa kikosi cha nchi kavu na Asad Qaiser, Spika wa Bunge la Pakistan.

Dakta Muhammad Javad Zarif aliwasili Islamabad mji mkuu wa Pakistan jana Alkhamisi akiuongoza ujumbe wa ngazi za juu wa Iran kwa shabaha ya kwenda kufanya mazungumzo na viongozi wa serikali mpya ya nchi hiyo lengo likiwa ni kupanua zaidi ushirikiano baina ya nchi mbili hizi.

Tags

Maoni