Sep 01, 2018 10:57 UTC
  • Madai ya hatari ya uwezo wa makombora ya Iran, propaganda zisizo na msingi

Uwezo wa makombora wa Iran ni jambo la kawaida katika medani ya masuala ya kijeshi na ni suala la kistratijia ambalo halipingani na sheria na kanuni za kimataifa kuhusu masuala ya silaha.

Uwezo huo hii leo ni moja kati ya nguzo muhimu za nguvu ya Jamhuri ya Kiislamu. Hii leo Iran, katika upande wa masuala ya ulinzi, ina uwezo wa kusimama kidete kukabiliana na upande wowote unaokusudia kuchafua na kuvuruga amani katika eneo la Mashariki ya Kati na kutoa jibu madhubuti kwa vitisho vya aina yoyote. Hata hivyo la kushangaza ni kuwa, baadhi ya nchi za Magharibi zimekuwa zikitoa madai na propaganda za uongo zikitaraji kuwa, Jamhuri ya Kiislamu itaacha kupanua na kustawisha zaidi uwezo wake kutokana na madai kama hayo. 

Katika mkondo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa amesema kuwa, Iran inapaswa kufanya mazungumzo na nchi za Magharibi kuhusu mipango yake ya makombora ya balestiki, harakati zake za kikanda na miradi yake ya nyuklia baada ya mwaka 2025. Madai kama hayo kwa upande mmoja yanafichua harakati kubwa ya propaganda za kudhihirisha uwezo wa makombora ya Iran kuwa ni "tishio" kwa amani ya kanda ya Mashariki ya Kati na dunia nzima, na kwa upande mwingine yana lengo la kuishinikiza Tehran na hatimaye kudhoofisha uwezo wake wa kujihami na kujilinda. 

Hii ni licha ya kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikisisitiza misimamo yake ya wazi kuhusu propaganda hizo chafu na ufahamu usio sahihi wa baadhi ya nchi kuhusiana na suala hilo. 

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Bahram Qassemi jana Ijumaa alijibu matamshi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian akisema: "Miradi ya makombora ya Iran ni kwa ajili ya kujihami, ni halali, ya kitaifa na kwa ajili ya kulinda nchi na raia wa Iran, na kamwe si suala la kujadiliwa kwenye meza ya mazungumzo."

Ukweli ni kwamba, hii leo na kutokana na vitisho mbalimbali vinavyoikabili Iran kikanda na kimataifa, statijia ya ulinzi imepata maana pana zaidi na kwa sababu hiyo Iran imekuwa ikipanua na kuzidisha uwezo wake wa kujihami kulingana na vitisho inavyokabiliana navyo.

Brigedia Jenerali Ali Reza Sabahifard ambaye ni kamanda wa kikosi cha Jeshi la Anga cha Khatamul Anbiyaa cha jeshi la Iran anasema: Viwanda vya zana za Jeshi la Anga la Iran sasa vimeondokana na hali ya kuwa tegemezi na kuanza kuzalisha zana za kisasa za ulinzi wa anga zenye viwango vya kimataifa.

Ayatullah Ali Khamenei

Vilevile Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei hivi karibuni alizungumzia makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na suala la kujiondoa Marekani katika makubaliano hayo ya kimataifa na kusisitiza kuwa, sharti la Iran kwa ajili ya kubakia katika makubaliano hayo ni kutohusishwa na miradi ya kutengeneza makombora ya Iran na ushawishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika eneo la Mashariki ya Kati.

Ni kwa msingi huo pia ndipo Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran akasema kuwa: "Viongozi wa nchi za Ulaya hadi sasa hawajaweza kutoa dhamana ya kutosha kwa ajili ya kulinda makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na suala hilo halibakishi sababu kuingia tena kwenye mazungumzo na nchi za Magharibi tena kwenye masuala ambayo hayajadiliki."

Kosa la kimahesabu la Marekani na nchi za Ulaya kuhusu uwezo wa makombora wa Iran na siasa zake za kikanda ni kwamba, pande hizo zinadhani kuwa, zinaweza kutumia makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kama wenzo na turufu ya kuibana Jamhuri ya Kiislamu katika meza ya mazungumzo. 

Shetani Mkubwa, Marekani, na wenzake wanataka kuidhoofisha Iran.

Alaa kulli hal, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kuwa: Sera za kikanda za Iran ni kuimarisha Amani na usalama wa kikanda na kimataifa na kupambana na ugaidi na misimamo ya kufurutu mipaka, na kama siasa hizo zinazikera na kuzikasirisha baadhi ya nchi zinazopendelea kuzusha ghasia na migogoro kwa ajili ya kudhamini maslahi yao haramu, basi ni muhimu kwao kurekebisha miendo na siasa zao.       

Maoni