Sep 03, 2018 10:50 UTC
  • Sifa za kipekee za kituo cha ulinzi wa anga Iran kwa mtazamo wa Kiongozi Muadhamu

"Kituo cha Ulinzi wa Anga cha Jeshi la Iran, ni sehemu muhimu ya majeshi kwani iko katika mstari wa mbele wa kukabiliana na maadui wa Iran."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyyed Ali  Khamenei aliyasema hayo Jumapili mjini Tehran alipokutana na kufanya mazungumzo na makamanda pamoja na maafisa wa ngazi za juu wa Kituo cha Ulinzi wa Anga cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran cha Khatamul Anbiya (SAW).

Kituo hiki kimekuwa kikiendeleza harakati zake kwa muda wa muongo mmoja sasa na kimeweza kupata mafanikio makubwa katika uga wa ulinzi wa anga kwa kutegemea wataalamu wa ndani ya nchi.

Hii leo weledi wengi wa mambo ya kijeshi na taasisi za kistratijia zimekiri kuhusu uwezo mkubwa wa utendaji wa majeshi ya Iran.

Sera za kijeshi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimejengeka katika msingi wa kujitegemea katika kuzalisha zana za kujihami kwa lengo la 'kuzuia adui kuanzisha uchokozi' na pia kwa jili ya 'kujihami kwenye ubunifu na athirifu'.

Katika fremu hii, Kituo cha Ulinzi wa Anga cha Jeshi la Iran kimeweza kustawi kwa kutegemea utaalamu wa ndani ya nchi na hivyo kuipa Iran uwezo wa juu wa kukabiliana na vitisho katika uga wa anga za juu na anga za mbali.

Mfumo wa Bavar 373

Kituo cha Utafiti wa Kistratijia cha American Enterprise  ambacho ni moja ya vituo maarufu na vyenye ushawishi nchini Marekani katika ripoti chini ya anuani ya "Mustakabali wa Sera za Usalama za Iran" kimeandika: "Shirika la Viwanda vya Ulinzi Iran ambalo lilianzishwa mwaka 1981 na wakuu wa Iran, pasina kununua silaha kutoka Marekani au Ulaya limekuwa likijishughulisha na uzalishaji, utafiti na ustawi wa sekta ya ulinzi nchini Iran. Wakati wahandisi Wairani walipofanikiwa kuunda makombora ya Scud, maghala ya makombora ya balistiki ya Iran yalibadilka na kuwa fahari kwa sekta ya ulinzi ya nchi hiyo."

Matthew McInnis mtaalamu wa masuala ya Iran katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani na ambaye pia alikuwa mtaalamu wa masuala ya Iran katika taasisi ya American Enterprise na Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani anafafanua zaidi kwa kusema: "Katika miaka ijayo, Iran itaweza kupata teknolojia za kisasa za kijeshi na kuna uwezekano nchi hii ikashuhudia mabadiliko ya hakika ya kijeshi."

Hivi sasa katika uga wa ulinzi wa anga, uwezo wa Iran umefika katika kiwango cha juu sana na ni ishara ya kasi ya ustawi na kuboreka kiwango cha mifumo ya ulinzi wa anga katika majeshi ya Iran.

Kwa mtazamo wa wataalamu, moja ya sifa za kipekee za Jeshi la Anga la Iran ni uwezo wa kutekeleza oparesehni athirifu za angani. Katika uga huu, Iran imezalisha mifumo yenye uwezo mkubwa ya ulinzi wa agani kama vile Mfumo wa Bavar 373,  mfumo wa masafa ya wastani wa ulinzi wa angani unaojulikana kama 'Mirsad' na mfumo wa masafa mafupi wa ulinzi wa angani  unaojulikana kama 'Zahra 3'.

Kwa mujibu wa jarida maarufu la ulinzi la 'Janes Defense' ambalo huchapishwa kwa lugha ya Kiingereza, hivi sasa Iran ina mifumo ya kisasa ya rada na mfano wake ni Rada ya '30N6' ambayo ni maalumu kwa kazi za upelelezi.

 

Ni kwa kuzingaitia uwezo huu ndio, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, sambamba na kubainisha kuhusu umuhimu wa kustawi Iran katika sekta za ulinzi, ametathmini zaidi kadhia hiyo kwa kusema: " Kwa mtazamo wa kisiasa, hakuna uwezekano wa kuanzishwa vita vya kijeshi dhidi ya Iran, lakini pamoja na hayo Majeshi ya Iran yanapaswa kuendelea kujiimarisha kwa mtazamo wa nguvu kazi, usimamizi bora na zana za kisasa za kivita.

Kwa msingi huo, kuimarisha uwezo na ustadi wa ulinzi wa anga, kupa kipaumbele  mipango ya kujihami na kuimarisha uwezo wa majeshi ya Iran kumzuia adui ni masuala yenye umuhimu kwa mtazamo wa stratejia ya kijeshi.

 

Tags

Maoni