Sep 06, 2018 10:17 UTC
  • Rais Donald Trump wa Marekani.
    Rais Donald Trump wa Marekani.

Mwakilishi wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa, Marekani ambayo ni mvunjaji mkubwa zaidi wa sheria za kimataifa inalitumia vibaya Baraza la usalama kwa ajili ya kupeleka mbele sera na mipango yake ya kujichukulia maamuzi ya upande mmoja.

Taarifa iliyotolewa na mwakilishi wa Iran katika Umoja wa Mataifa kujibu matamshi ya mwakilishi wa Marekani katika umoja huo, Nikki Haley juu ya kuitishwa kikao cha Baraza la Usalama kitakachojadili Iran imesema: Marekani inatumia vibaya nafasi na uanachama wake wa kudumu katika Baraza la Usalama na kama mwenyekiti wa sasa wa baraza hilo kuyatwisha mataifa mengine maamuzi yake ya upande mmoja na hatua hiyo ni kutekeleza sera za kutumia mabavu, vitisho na ubabe katika mahusiano ya kimataifa. 

Imepangwa kuwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litaitisha kikao tarehe 26 mwezi huu wa Septemba kujadili Iran. Kikao hicho kitaongozwa na Rais Donald Trump wa Marekani. Baada ya Trump kuingia White House, Marekani imezidisha uhasama na uadui dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kiongozi huyo amekuwa akitumia majukwaa yote kwa ajili ya kuiarifisha Iran kuwa ndiyo sababu ya machafuko na ukosefu wa amani katika eneo la magharibi mwa Asia. Trump anatumia majukwaa hayo kupeleka mbele sera zake za kueneza propaganda chafu dhidi ya Iran. Serikali ya Marekani inatumia pia siasa hizo za kueneza propaganda chafu dhidi ya Iran kama kifuniko cha kuwasahaulisha walimwengu maudhui kuu ya Mashariki ya Kati yaani uvamizi wa Wazayuni na kukaliwa kwa mabavu ardhi ya Palestina na kuukingia kifua utawala bandia na ghasibu wa Israel. Hatua ya Trump ya kuhamishia ubalozi wa Marekani katika mji unaokaliwa kwa mabavu wa Quds kutoka Tel Aviv na jitihada zake za kutaka kufunga kabisa Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada na Ajira kwa Ajili ya Wapalestina (UNRWA) vinatathminiwa kuwa ni sehemu ya mpango habithi uliopewa jina la Muamala wa Karne na sasa kiongozi huyo wa Marekani anashirikiana na baadhi ya nchi za Kiarabu kama Saudi Arabia kutekeleza mpango huo sambamba na kueneza chuki na propaganda chafu dhidi ya Iran.

Image Caption

Mbali na hayo vitisho vinavyotolewa na Marekani dhidi ya nchi mbalimbali na kuzitaka zikate uhusiano wao wa kiuchumi na Iran baada ya Washington kujiondoa katika makubaliano ya kimataifa ya nyuklia ya JCPOA ni kielelezo cha siasa na sera za kutumia mabavu katika siasa za kimataifa. Mwakilishi wa Iran katika Umoja wa Mataifa, Gholamali Khoshrou alikiambia kikao cha Baraza la Usalama Jumatano iliyopita kwamba: Dunia ipaswa kuongozwa kwa sheria na si kwa kutumia mabavu na moja kati ya mifano ya sera za utumiaji mabavu za Marekani ni ukiukaji wake wa azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuzihamasisha nchi nyingine kuasi azimio hilo la sivyo zitakabiliwa na adhabu kali.

Kwa hakika mashinikizo yote ya serikali ya Trump dhidi ya Iran ni kielelezo cha kupamba moto sera za uhasama wa Marekani dhidi ya Iran ambayo ni nchi inayojitawala na inayowajibika na kutoa changamoto kwa siasa za kibeberu za serikali ya Washington. Iran ambayo ina ustaarabu na utamaduni wa maelfu ya miaka inatambuliwa kama nchi inayopenda amani duniani. 

Ayatullah Ali Khamenei

Itakumbukwa kwamba, tarehe 13 Agosti Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei aliiambia hadhara kubwa ya wananchi kwamba: Viongozi waliotangulia wa Marekani hawakuwa na adabu ya kisiasa wala ya kidiplomasia katika matamshi yao lakini hawa wa sasa wamewazidi kwa kuzungumza na walimwengu kwa kutumia lugha isiyo na adabu na bila ya kuona haya

Tags

Maoni