Sep 08, 2018 11:30 UTC
  • Uhusiano wa kistratejia kati ya Iran, Uturuki na Russia kwa mtazamo wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Ayatullah Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu jana alasiri alikutana na kufanya mazungumzo na Rais Rajab Tayyeb Erdogan wa Uturuki na ujumbe aalioongozana nao hapa Tehran na kusema kuwa hitajio muhimu zaidi la ulimwengu wa Kiislamu hii leo ni kukurubiana zaidi nchi za Kiislamu na kushikamama nchi hizo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi amebainisha kuwa ubeberu ukiongozwa na Marekani una wasiwasi mkubwa kuhusu ushirikiano na kukaribiana nchi za Kiislamu na kujitokeza nguvu kubwa ya Kiislamu duniani. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema uadui na chuki ya Marekani  dhidi ya nchi za Kiislamu zilizo na nguvu unatokana na wasiwasi huo na kuongeza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Uturuki ni nchi mbili zinazoheshimika, zenye nguvu katika eneo na zilizo na malengo ya pamoja kwa ajili ya ulimwengu wa Kiislamu. Kwa msingi huo ushirikiano wa nchi mbili katika nyanja za kisiasa na kiuchumi unapasa kuimarishwa zaidi na zaidi.  

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu jana usiku pia alifanya mazungumzo na Rais Vladimir Putin wa Russia na ujumbe aliofuatana nao hapa Tehran na kusisitiza kuwa: Ushirikiano wa nchi mbili za Iran na Russia unaweza kuimarishwa pia katika mgazi za kimataifa. Ayatullah Khamenei ameutaja mtazamo wa Rais wa Russia kuhusu makubaliano ya JCPOA pia kuwa ulio na nia njema na kubainisha kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itachukua uamuzi kuhusu makubaliano ya JCPOA kwa maslahi na kwa ajili ya izza ya nchi na watu wake. Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa hata kama viongozi wa Marekani sasa wanazungumza kuhusu makombora ya Iran na masuala mengine katika eneo, lakini suala kuu lililoko baina yao na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni zaidi ya masuala haya. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Ni miaka 40 sasa ambapo viongozi wa Marekani wanataka kuing'oa mizizi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lakini sisi katika kipindi chote hiki tumepiga hatua mara arubaini zaidi; ambapo ni kusimama imara huku kwa Jamhuri ya Kiislamu na mafanikio yake ndiko kunachukuliwa kuwa mfano mwingine wa wazi wa kushindwa Marekani kukabiliana na Iran. 

Ayatullah Khamenei katika mazungumzo na Rais Putin wa Russia mjini Tehran

Hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mazungumzo na Rais wa Uturuki na vile vile Rais wa Russia ni dhihirisho la uhakika wa mambo, fursa na mahitaji ya sasa katika eneo hili. Hata hivyo kustafidi na fursa zilizopo khususan katika vipindi nyeti na muhimu kama mazingira yaliyopo sasa katika eneo la Mashariki ya Kati kunahitajia ushirikiano wa pande kadhaa. Uzoefu wa ushirikiano wa kistratejia kati ya Iran, Russia na Uturuki katika mapambano dhidi ya Daesh na ugaidi huko Syria, na vikao vya pande tatu vya jana Ijumaa kati ya Marais wa Iran, Russia na Uturuki hapa Tehran unaonyesha kuwepo nguvu kubwa katika umoja huo, ambayo iwapo itatumiwa vizuri inaweza kupelekea kutatuliwa matatizo mengi yaliyopo na nchi hizo kusimama imara mkabala na mashinikizo na vitisho vya pamoja. Moja ya fursa kubwa katika uwanja huo ni kustafidi na suhula na uwezo wa Iran na nchi jirani zake zikiwemo Uturuki na Russia ili kuweza kukabiliana na vitisho vinavyohatarisha usalama wa pamoja na hata uchumi wa nchi za eneo. 

Magaidi wa kundi la kitakfiri la Daesh 

Kama alivyotilia mkazo nukta hii Kiongozi Muadhamu Marekani kuziwekea vikwazo Iran, Russia na Uturuki ni nukta ya pamoja na yenye nguvu kwa ajili ya kupanua ushirikiano kati ya nchi hizo na kuongeza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Russia zinapasa kuimarisha ushirikiano wa kisiasa na kiuchumi kati ya pande mbili na kufuatilia kwa karibu makubaliano yaliyofikiwa katika kikao cha Tehran. 

Ameongeza kuwa moja ya masuala ambayo pande mbili zinaweza  kushirikiana kwa pamoja ni kuidhibiti Marekani kwa sababu Marekani ni hatari kwa ubinadamu na uwezekano wa kuidhibiti pia upo. 

Vikao kama hivi ambavyo vinatoa taswira chanya kuhusu umoja ulioko baina ya Russia, Uturuki na Iran vinatoa matarajio ya kuimarishwa ushirikiano wa kieneo na vinaweza kuwa changamoto pia kwa hatua na misimamo ya upande mmoja ya Marekani.  

Kwa mtazamo huo, hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi alipokutana na marais wa Uturuki na Russia inaonyesha umuhimu wa ushirikiano wa kistratejia  uliopo kati ya nchi tatu hizi katika masuala ya kisiasa, kijeshi na kiuchumi katika eneo. 

Maoni