Sep 09, 2018 07:49 UTC
  • Iran: Marekani inayatumia makundi ya kigaidi kufikia malengo yake

Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Marekani inatumia njia zote kukiwemo kuyatumia makundi ya kigaidi kufikia malengo yake pasina kujali madhara kwa nchi nyingine.

Brigedia Jenerali Amir Hatami ameyasema hayo katika mazungumzo yake na Naibu Mwenyekiti wa Kamisheni Kuu ya Kijeshi ya China (CMC), Jenerali Zhang Youxia katika mji mkuu wa nchi hiyo ya Asia, Beijing.

Ameongeza kuwa, kukiuka sheria na kanuni za kimataifa, kuanzisha vita vya kibiashara, kukiuka makubaliano ya kimataifa kama vile mapatano ya nyuklia ya Iran JCPOA na makubaliano ya mabadiliko ya tabianchi ya Paris, ni miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na Marekani bila kujali kuwa inakiuka mfumo wa kimataifa wa usalama.

Hatami na Zhang Youxia

Brigedia Jenerali Amir Hatami amebainisha kuwa, ugaidi, misimamo mikali ya kufurutu ada, harakati za kujitenga na uingiliaji wa masuala ya ndani ni miongoni mwa mambo ambayo yamesababisha kushtadi migogoro duniani na hususan katika eneo la Mashariki ya Kati.

Katika mkutano huo na Naibu Mwenyekiti wa Kamisheni Kuu ya Kijeshi ya China (CMC), Jenerali Zhang Youxia, afisa huyo wa ngazi za juu wa Iran amesema magenge ya kigaidi nchini Syria yanaelekea kusambaratika kutoka na jitihada za Iran, Russia na harakati ya Hizbullah ya Lebanon. 

 

Tags

Maoni