Sep 09, 2018 16:13 UTC
  • Amiri Jeshi Mkuu: Taifa la Iran limeirudisha nyuma na kuishinda Marekani

Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi yote ya Iran amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu na taifa la Iran limethibitisha kwa kusimama kidete mbele ya Marekani kwamba, iwapo taifa lolote halitaogopa hasira na ghadhabu za mabeberu na kuamini na kutegemea uwezo wake, madola makubwa yatarudi nyuma na hatimaye kushindwa.

Ayatullah Ali Khamenei ambaye alikuwa akizungumza kwenye sherehe ya kuapishwa wanafunzi wa vyuo vikuu vya maafisa wa jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ameashiria siasa za kishetani za madola ya kibeberu za kuzusha machafuko na ukosefu wa usalama katika eneo la Mashariki ya Kati na kusema kuwa: Mabeberu wakiongozwa na Marekani dhalimu, wanayaona maslahi yao kuwa yamo katika kuanzisha vita vya ndani, kuzidisha harakati za kigaidi na mapigano ya kikanda na inasikitisha kuona baadhi ya nchi za eneo hili zikiwasaidia.

Amir Jeshi Mkuu amesema kuwa lengo la Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel ni kuzuia kuwepo dola kubwa la Kiislamu katika eneo la Mashariki ya Kati na kuongeza kuwa: Mabeberu hao wanajua vyema kwamba, ujumbe unaovutia watu wa Uislamu ni kuwatetea watu wanaodhulumiwa na kukandamizwa; kwa msingi huo wana woga na hofu ya kuwepo dola lenye nguvu lililoanzishwa kwa misingi ya Uislamu. 

Ayatullah Khamenei amesema kuwa kusimama kidete kwa Jamhuri ya Kiislamu mbele ya ubeberu kumepelekea kushindwa malengo mengi ya madhalimu wa kimataifa katika eneo hili. Ameongeza kuwa: Wachambuzi wa siasa na weledi wa mambo duniani wamebakia bumbuazi kuona Iran ikiyashinda madola makubwa katika siasa zao zinazohusiana na Mashariki ya Kati kutokana na kumtegemea Mwenyezi Mungu na kuegea kwenye nguvu zake za kitaifa. 

Amiri Jeshi Mkuu akikagua gwaride la jeshi.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa: Katika kipindi chote cha miaka 40 iliyopita Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikikabiliwa na wimbi kubwa la uharifu wa Marekani na washirika wake lakini sasa imebadilika kutoka mche mchanga na kuwa mti imara na wenye matunda; na licha ya njama zinazofanywa na mabeberu, imefanikiwa kuzivutia nyoyo za mataifa mbalimbali kwenye ujumbe wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuzishinda njama za Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati.

Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi yote ya Iran amesema kuwa Syria, Iraq na Lebanon ni mfano wa kushindwa siasa za Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati na kuongeza kuwa: Hizi ni ishara za nguvu ya Mwenyezi Mungu na vielelezo vya kutimia ahadi za Allah ambaye anasema: Mkimnusuru Mwenyezi Mungu naye atakunusuruni na ataithabitisha miguu yenu.  

Tags

Maoni