Sep 10, 2018 03:37 UTC
  • Iran katu haitafanya mazungumzo kuhusu uwezo wake wa makombora

Mshauri wa Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi Yote ya Iran katika masuala ya viwanda vya kijeshi amesisitiza kuwa: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitafanya mazungumzo kuhusu uwezo wake wa makombora."

Brigedia Jenerali Hussein Dehqan ameyasema hayo katika mahojiano na Televisheni ya Rosiya al Youm na kuongeza kuwa, uwezo wa makombora ya Iran ni suala la nguvu, heshima, uhuru na kujiamini taifa na hivyo suala hilo si la kuwekwa mezani kufanyiwa mazungumzo.

Brigedia Jenerali Dehqan amesema: "Marekani, Israel na Saudi Arabia zinaongoza na kuratibu fitina kubwa katika eneo." Aidha amebaini kuwa tawala hizo tatu hazina uwezo wa kuingia katika vita vya moja kwa moja na Iran.

Dehqan ambaye aliwahi kuwa waziri wa ulinzi wa Iran ameendelea kusema kuwa,  watu wa Yemen wamedhulumiwa na hivi sasa wanakabiliwa na hujuma ya kigeni na kwa msingi huo amesema, "iwapo Wayemen wataomba msaada, Iran itawasaidia."

Brigedia Jenerali Hussein Dehqan

Brigedia Jenerali Dehqan ameashiria hali ya mambo huko Idlib nchini Syria na kuongeza kuwa: "Magaidi hawapaswi kuachwa kufanya wanalotaka na kuenda sehemu yoyote wanayotaka bali inapaswa kukabiliana na magaidi na kuwaangamiza."

Brigedia Jenerali Dehqan amebaini kuwa: "Serikali ya Syria haijaiomba Marekani itume wanajeshi wake nchini humo na hivyo Marekani inapaswa kuondoka Syria mara moja.

Tags

Maoni