Sep 10, 2018 06:53 UTC
  •  Kiongozi Muadhamu asisitiza kuimarishwa uwezo wa majeshi ya Iran katika kukabiliana na adui

Ayatullah Sayyed Ali Khamenei, Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi Yote ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran jana alishiriki katika mahafali ya pamoja ya kuhitimu na kuapishwa wanafunzi wa vyuo vikuu vya maafisa wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuashiria sera za shari na kiistikbari za kuibua machafuko na ukosefu wa usalama na kusisitiza kuwa:

"Mabeberu wakiongozwa na Marekani dhalimu, wanayaona maslahi yao yakiwa katika kuanzisha vita vya ndani, kuzidisha harakati za kigaidi na mapigano ya kikanda na inasikitisha kuona baadhi ya nchi za eneo hili zikiwasaidia." Amir Jeshi Mkuu amesema kuwa lengo la Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel ni kuzuia kuwepo dola kubwa la Kiislamu katika eneo la Mashariki ya Kati na kuongeza kuwa: Mabeberu hao wanajua vyema kwamba, ujumbe unaovutia watu wa Uislamu ni kuwatetea watu wanaodhulumiwa na kukandamizwa; kwa msingi huo wana woga na hofu ya kuwepo dola lenye nguvu lililoanzishwa kwa misingi ya Uislamu. 

Kiongozi Muadhamu aliongeza kuwa: "Hatua ya Jamhuri ya Kiislamu ya kusimama kidete na wazi wazi mbele ya udhalimu na ubeberu ndio sababu kuu ambayo imepelekea madhalimu duniani wahasimiane na  taifa kubwa la Iran."

Jeshi la wanamaji la Iran,  hivi sasa linatuma manowari  na kuonyesha uwezo wake katika maeneo muhimu kama vile Bahari ya Makran, Bahari ya Oman na maeneo mengine ya baharini katika maji ya kimataifa.  Hivi sasa jeshi hilo linalinda usalama katika Ghuba ya Uajemi, Bahari ya Oman na Bahari ya Hindi na linaweza kufika eneo lolote lile katika maji ya kimataifa ambalo linahitaji usalama.

Brigedia Jenerali Amir Hatami, Waziri wa Ulinzi wa Iran katika ujumbe alioutuma kwa mnasaba wa Siku ya Jeshi la Majini, aliashiria uwezo mkubwa wa Jeshi la Majini la Iran na kusema: "Jeshi la Majini la  Jamhuri ya Kiislamu ya Iran  likiwa linashirikiana kwa karibu na Jeshi la Majini la Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, IRGC, limeweza kupata nguvu mpya iliyodhihiri katika uga wa usalama wa bahari katika mipaka ya nchi na pia nje ya nchi."

Kiongozi Muadhamu akikagua gwaride

Uzoefu wa karibu karne moja iliyopita umeonyesha kuwa moja kati ya malengo ya Marekani ni kugonganisha mataifa kwa kuibua migogoro isiyo na msingi kupitia kujipenyeza na kuingilia kijeshi nchi zingine sambamba na kuzidisha vitisho katika eneo. Lengo la Marekani ni kueneza satwa yake ya kibeberu katika maeneo muhimu na ya kistratijia, kuhakikisha nchi za eneo zinategemea madola ajinabi kudhaminia usalama wao. Aidha Marekani inalenga kuhakikisha kuwa inauzia nchi za eneo idadi kubwa ya silaha zenye thamani ya mabilioni ya dola pamoja na kuendelea kuwepo katika eneo hili vituo vyake vya kijeshi.

Kwa msingi huo, vitisho viliyvopo vinailazimu Iran iendelee na kasi ya kuimarisha uwezo wake wa ulinzi.

Hotuba ya jana ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa hakika inasisitiza kuhusu kuimarishwa harakati ya kuongeza nguvu ya majeshi ya Iran ili kukabiliana na vitisho vya maadui.

Kinadharia, kila nchi huru na yenye kujitegemea hata kama iko katika eneo lenye usalama na amani inapaswa kuwa na uwezo mkubwa wa kijeshi wa kuzuia mashambulio ya adui na kujilinda.

Vikosi vya ulinzi vya Iran, wakati wowote ilipolazimika, vimewaonyesha maadui kuwa nchi hii una uwezo unaohitajika wa kuzuia na kukabiliana na vitisho.

Kama ambavyo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi alivyosema katika hotuba yake: "Jamhuri ya Kiislamu na  taifa la Iran kwa kusimama kidete mbele ya ubabe wa Marekani limethibitisha kuwa, iwapo taifa halitaogopa vitisho vya madola yanayotumia mabavu, na iwapo litaweza kujiamini na kujitegemea, basi litapelekea madola ya kibeberu yarudi nyumba na hatimaye kushindwa.

Maafisa wa Jeshi la Majini la Iran katika mahafali ya kuhitimu

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema Syria, Iraq na Lebanon ni mifano ya wazi ya kufeli njama za Marekani katika eneo.

Ni kwa msingi huo ndio Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi Yote ya Iran katika sehemu ya hotuba yake ya jana akashauri majeshi nchini yaimarishe harakati za ubunifu, utayarifu na uwezo katika medani za sayansi, usimamizi, kivita na kila aina ya ustawi unaohitajika. Ameongeza kuwa: Kwa mujibu wa aya ya Qur'ani Tukufu, waumini wanapaswa kuimarisha uwezo  wao kadiri inavyowezekana na uwezo huo utawaingiza hofu maadui na kuwalazimisha kurudi nyuma."

Majeshi ya majini ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yanafuatilia lengo hilo na yameweza kuimarisha nafasi yake na kuwa jeshi la kistratijia la majini na muelekeo huu una thamani na umuhimu mkubwa kwa nchi ambazo zinataka kuwa na usalama wa kudumu.

Tags

Maoni