Sep 10, 2018 14:42 UTC
  • IAEA: Iran imetekeleza makubaliano ya JCPOA

Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) umetoa taarifa leo ukitangaza tena kwamba, Iran imetekeleza majukumu na ahadi zake zote chini ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Taarifa ya wakala huo iliyotolewa mjini Vienna Austria imesema kuwa IAEA itaendeleza ushirikiano wake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. 

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, Yukia Amano amesema katika hotuba ya ufunguzi wa mkutano wa Baraza la Magavana wa Wakala wa IAEA kwamba Iran inaendelea kutekeleza majukumu yake ndani ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA. 

Mkutano wa msimu wa Baraza la Mavana wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki umefunguliwa leo mjini Vienna. Masuala yanayojadiliwa katika mkutano huo wa siku tano ni pamoja na hatua za kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika masuala ya nyuklia, usafirishaji na usalama wa taka za nyuklia. 

Mkutano wa wakala wa IAEA, Vienna.

Ripoti za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki zimekuwa zikisisitiza kuwa Iran imetekeleza na kuheshimu vipengee vyote vya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yaliyotiwa saini na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi za kundi la 5+1. 

Rais Donald Trump wa Marekani tarehe 8 Mei mwaka huu aliiondoa nchi hiyo katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, suala ambalo limekabiliwa na upinzani mkubwa wa nchi nyingine zilizoyatia saini.   

Tags

Maoni