Sep 11, 2018 04:18 UTC
  • Shamkhani: Iran haitasalimu amri mbele ya dhulma na uonevu

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesema kuwa, taifa la Iran kamwe halitasalimu amri mbele ya dhulma, uonevu na udhalilishaji na litawadunisha maadui na wanaolitakia mabaya.

Ali Shamkhani amesema kuwa, lengo la vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran ni kubana uwezo na nguvu ya taifa la Iran na kuongeza kuwa, taifa la Iran linaweza kustawisha uchumi wake kama ilivyo katika sekta ya ulinzi na usalama.

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesema kipindi cha "kupiga na kukimbia" kimepita na kwamba uadui wa aina yoyote dhidi ya Iran utapatiwa jibu kali.

Ali Shamkhani

Shamkhani amesema kuwa, mashambulizi ya makombora yaliyofanywa hivi karibuni dhidi ya kundi la kigaidi katika eneo la Kurdistan nchini Iraq yalikuwa jibu la harakati za kuvuruga amani za kundi hilo katika maeneo ya mpakani ya Iran. Amesisitiza kuwa mwenendo huo utaendelea dhidi ya vitisho vya aina hiyo.

Itakumbukwa kuwa, Jumamosi iliyopita Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu lilishambulia kwa makombora saba ya masafa mafupi makao na mkutano wa viongozi wa kundi moja la kigaidi na vilevile kituo chao cha mafunzo katika eneo la Kurdistan nchinI Iraq.  

Tags

Maoni