Sep 11, 2018 07:32 UTC
  • Kharrazi: Aghalabu ya nchi duniani zinapinga sera za Marekani dhidi ya Iran

Mkuu wa Baraza la Stratejia za Uhusiano wa Nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: Marekani inatekeleza sera zake dhidi ya Iran kwa kutumia mabavu, ubabe na vitisho.

Kamal Kharrazi ameyasema hayo katika kikao kilichofanyika kwenye chuo kikuu cha Taaluma za Kimataifa cha Beijing nchini China kwa anuani ya "Sera za Nje za Iran Katika Hali ya Sasa".

Amesema madamu hakuna mabadiliko katika malengo ya Marekani na madamu utawala huo unaendeleza vitisho na ubabe dhidi ya wananchi na Mfumo wa utawala wa Iran, Tehran haiko tayari kufanya mazungumzo ya aina yoyote na Marekani.

Mkuu wa Baraza la Stratejia za Uhusiano wa Nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa viongozi wa Marekani wanaziona nchi kama Iran, China, Russia na hata baadhi ya waitifaki wao wa Ulaya kuwa ni hatari kwa satua ya Washington duniani kwa hivyo kwa mtazamo wao wao harakati za kisiasa na kijeshi na ushawishi wa kieneo wa nchi zingine havipasi kuwa kikwazo kwa satua ya Marekani duniani.

Dakta Kharrazi amebainisha kuwa ili kuonesha nia njema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikubali kufanya mazungumzo na nchi zilizounda kundi la 5+1 lililotokana na ubunifu wa Marekani yenyewe na hatimaye yakafikiwa makubaliano ya JCPOA.  Ameongezea kwa kusema: Kwa mujibu wa ripoti za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA), hadi sasa Iran imetekeleza yale yote yaliyoafikiwa kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, lakini baada ya kutokea mabadiliko ya serikali nchini Marekani na kushika hatamu za utawala kundi lenye misimamo ya kufurutu mpaka nchi hiyo imejitoa kwenye JCPOA na kuamua kuiwekea vikwao vyengine vipya Iran huku ikizilazimisha nchi nyingine ziungane nayo katika kuishinikiza Iran.

Mkuu wa Baraza la Stratejia za Uhusiano wa Nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza kuwa utumiaji huo mabavu na uchukuaji hatua haramu unaofanywa na Marekani ambao lengo lake ni kuwadhuru wananchi na Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katu hauwezi kuvumiliwa na akasisitiza kwamba Iran itafanya kila iwezalo kwa msaada wa marafiki zake kukabiliana na hali hiyo.../

Tags

Maoni