Sep 11, 2018 10:00 UTC
  • Makubaliano ya Iran na Russia; kukabiliana na hatua za chuki na vikwazo vya Marekani

Serikali ya Russia ina hamu na shauku ya kuimarisha zaidi ushirikiano wake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hususan katika uga wa biashara na uchumi.

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Russia ilitoa taarifa rasmi jana  na kutangaza kuwa, katika mazunguumzo ya Sergei Ryabkov, Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia na Abbas Araqchi, Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran yaliyofanyika mjini Tehran, Moscow na Tehran  zimekubaliana kutoa dhamana ya kuendeleza mwenendo wa kibiashara wa pande mbili kwa minajili ya kukabiliana na hatua za chuki na vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran.

Kwa mujibu wa tangazo la Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Russia, Moscow imesisitiza katika mazungumzo hayo juu ya kufungamana kwake na makubaliano ya nyuklia ya Iran hasa kwa kutilia maanani umuhimu huu kwamba, Tehran imetekeleza ahadi zake kwa mujibu wa makubaliano hayo ya JCPOA.  Ushirikiano wa Iran na Russia umechukua mkondo mpana zaidi na kujumuisha sekta mbalimbali kama ujenzi wa vituo vya nishati, utalii, usafiri na uchukuzi na  usafiri wa meli. Ushirikiano huu umekuwa na nafasi muhimu sana katika kupanua ushirikiano wa kiuchumi baina ya pande mbili. 

Marais wa Iran, Russia na Uturuki walipokutana 07.09.2018 mjini Tehran katika mkutano wa pande tatu

Katika uga huo, kumependekezwa fikra kama kuundwa Umoja wa Kibiashara wa Iran na Russia ambayo inafuatiliwa na Chama cha Wafanyabiashara na Wenye Viwanda cha Russia na Baraza la Biashara  la Iran na Russia. Makubaliano yaliyofikiwa jana mjini Tehran nayo kwa namna fulani yanabainisha kuweko mfungamano wa kisiasa na kiuchumi katika ushirikiano wa pande mbili na ushirikiano wa kiistratejia baina ya Iran na Russia.

Upande muhimu wa makubaliano ya Iran na Russia ni kuweko mtazamo mmoja katika uhusiano wa kibiashara wa Iran na Russia wenye lengo la kukabiliana na vikwazo vya Marekani. Abdolrasoul Divsalar, mtaalamu wa masuala ya Russia anaamini kwamba: Kushtadi ushindani wa kieneo na kuweko siasa zenye kuzusha changamoto za Marekani na baadhi ya madola ya Ulaya, kumepelekea kupewa umuhimu zaidi uhusiano wa Russia na Iran.

Bendera za Iran na Russia

Weledi wa masuala ya kisiasa wanaamini kwamba, kutokana na uwezo na fursa zilizopo katika uhusiano wa Iran na Russia, muda si mrefu unaweza kushuhudiwa uhusiano thabiti na imara zaidi baina ya nchi mbili hizi na kwamba hivi sasa umewadia wakati wa kunufaika na uwezo huo.

Morteza Khansari, mtaalamu wa masuala ya kimataifa anaamini kwamba, kutokana na Iran na Russia kuwa na akiba kubwa ya nishati ya mafuta na gesi, zinaweza kuwa na nafasi muhimu na ya kuzingatiwa katika suala zima la uongozi na udhamini wa usalama wa nishati duniani na kuuongoza ulimwengu upande wa mfumo wa kambi mbili unaoungwa mkono na mataifa mengi ya dunia.

Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ijumaa iliyopita alisema katika mazungumzo yake hapa mjini Tehran na Rais Vladmir Putin wa Russia pamoja na ujumbe aliofuatana nao kwamba: Kuwekewa vikwazo Iran, Uturuki na Russia kulikofanywa na Marekani ni nukta chanya mno kwa ajili ya ushirikiano wa nchi hizo ili kustawisha zaidi ushirikiano na kuongeza kuwa, Iran na Russia sanjari na kupanua ushirikiano wa kisiasa na kiuchumi zinapaswa kufuatilia kwa uzito mkubwa makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano wa pande tatu wa Tehran.

Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu akifanya mazungumzo  na Rais Vladmir Putin wa Russia 

Aidha Kiongozi Muadhamu alitilia mkazo suala la kutotumia sarafu ya dola katika miamala na mabadilishano ya kiuchumi. Rais wa Russia kwa upande wake alisema bayana kwamba: Wamarekani wanafanya kosa la kiistratijia kwa hatua yao ya kuweka mipaka na udhibiti katika mabadilishano ya kifedha, kwa sababu tu ya kutaka kupata mafanikio ya kisiasa na ya muda mfupi. Hatua hiyo itawafanya watu wasiwe na imani na sarafu ya dola katika anga ya kimataifa na matokeo yake ni kudhoofika dola. 

Kwa hakika majimui ya masuala haya ni ishara ya wazi kwamba, uhusiano wa Iran na Russia katika uga wa uchumi umekuwa kama ilivyokuwa katika suala la mitazamo mimoja ya kisiasa. Mwenendo huu unaweza kuwa wenzo mwafaka kwa ajili ya kuimarisha uhusiano baina ya nchi mbili hizi.

Maoni